Featured Kitaifa

MPANJU:AJENDA YA MALEZI NI MTAMBUKA WADAU TUSHIRIKIANE

Written by Alex Sonna

WMJJWM – Dodoma

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju amesema suala la malezi ni ajenda mtambuka inayohitaji nguvu na ushirikiano wa Wizara, Taasisi za dini, jamii na wadau wa maendeleo.

Wakili Mpanju amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya majaribio ya kitini cha mwezeshaji wa uanzishaji na uendeshaji wa vikundi vya wazazi vya malezi na matunzo ya watoto jijini Dodoma, tarehe 29 Septemba, 2025.

Wakili Mpanju, amesema lengo kuu ni kufanya majaribio ya awali ya kitini hicho pamoja na kukijadili na kutoa maoni yatakayosaidia kuboresha muongozo huo ambapo kitini hicho kinatarajiwa kuwa nyenzo muhimu ya kuelimisha wazazi na walezi kuhusu malezi chanya, ulinzi wa mtoto, lishe na afya ya mama na mtoto

“Kitini hiki kimeandaliwa kwa lengo la kusaidia wazazi na walezi kupata elimu ya malezi chanya na kitaendelea kutumika kuwajengea uwezo wawezeshaji katika ngazi mbalimbali za jamii.” amesisitiza Wakili Mpanju

Aidha amewataka washiriki wa mafunzo hayo kulitumia ipasavyo kitini hicho pamoja na zana mpya ya ukusanyaji taarifa (Parenting Collection Tool), ili kuimarisha vikundi vya wazazi na kueneza elimu chanya kwa jamii.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto, Sebastian Kitiku, amesema kitini hicho kimebeba dira ya taifa ya kuhakikisha kila mzazi au mlezi anapata mwongozo sahihi wa malezi huku akisisitiza kuwa kinatoa mbinu rahisi na zinazotekelezeka hata katika mazingira ya vijijini na hivyo kitakuwa nyenzo ya kuondoa tofauti katika upatikanaji wa elimu ya malezi nchini.

Kitiku ameongeza kuwa maoni ya washiriki yatakayokusanywa kupitia mafunzo hayo yatasaidia kukiboresha kitini hicho kabla ya kupelekwa kwa matumizi ya kitaifa.

Baadhi ya washiriki wa kikao hicho wameahidi kuyatumia mafunzo hayo kama mwongozo wa vitendo watakaporejea kwenye jamii zao kwa lengo la kuanzisha au kuimarisha vikundi vya wazazi na walezi ili kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama na yenye malezi bora.

About the author

Alex Sonna