Featured Kitaifa

MENEJA TRA WILAYA YA BAHI ASISITIZA USAJILI WA TIN NA MALIPO YA KODI AWAMU YA TATU

Written by Alex Sonna

 

Na. Yahya Saleh-Bahi

Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma Bw. Emmanuel Nyeme amewataka Wafanyabiashara na Walipakodi kwa ujumla ambao hawajasajiliwa kufanya hivyo kwani ni kinyume cha sheria kufanya biashara bila kuwa na Namba ya Utambilisho wa Mlipakodi (TIN).

Pia, amewakumbusha kulipa malipo ya kodi ya awamu ya tatu kabla ya tarehe 30 Septemba, 2025.

Hayo ameyazungumza leo Jumatatu tarehe 29.09.2025 wakati wa zoezi la elimu ya kodi mlango kwa mlango katika Wilaya ya Bahi.

“Ni kinyume cha sheria kufanya biashara bila ya kuwa na Nambari ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN)”, alisema Bw. Nyeme.

Aidha, amewasisitiza wafanyabiashara kutoa Risiti za kielektroniki kwa wateja wao pale wanapofanya manunuzi huku akiwahimiza wananchi nao kudai risiti pale wanaponunua bidhaa au huduma kutoka kwa Wafanyabiashara.

Kwa upande wao Wafanyabiashara Wilayani Bahi waliotembelewa katika zoezi hilo, wameipongeza TRA kwa kuja na kampeni hiyo huku wakiomba zoezi hilo liwe endelevu.

About the author

Alex Sonna