Mgombea urais kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo, ameahidi kuboresha miundombinu ya barabara na nishati katika Jiji la Mwanza na mikoa yote ya Kanda ya Ziwa endapo atachaguliwa kuongoza nchi.
Akihutubia wananchi wa Mwanza kwenye mkutano wa kampeni, Doyo alisema barabara kuu ya Mwanza–Shinyanga itapanuliwa na kujengwa kwa kiwango cha lami kuwa barabara mbili za kisasa ili kupunguza ajali na kurahisisha usafiri.
“Kwa heshima ya Jiji la Mwanza, tunapaswa kulifanya kitovu cha utalii na biashara. Utalii na biashara vitachochea ukuaji wa uchumi wa wananchi. Tunataka wafanyabiashara wafike Mwanza na kusafiri kwa urahisi ili kuharakisha mzunguko wa uchumi,” amesema Doyo
Ameongeza kuwa ipo haja ya kujenga barabara za juu (flyover) katika maeneo yenye msongamano mkubwa, ikiwemo Rock City, ili kupunguza foleni na kurahisisha shughuli za kila siku.
“Tunakwenda kujenga barabara za juu ili kuondoa foleni kama ilivyo kwenye majiji mengine. Hii itawawezesha wananchi kuendelea na majukumu yao na kuchangia pato la taifa. Ni busara kumtengenezea Mtanzania mtandao rahisi wa ulipaji kodi,” amesisitiza.
Aidha, Doyo ameahidi kuwa serikali ya NLD itajenga kituo kikubwa cha kuzalisha umeme ndani ya Ziwa Victoria chenye uwezo wa kuzalisha zaidi ya megawati 2,000 ili kuondoa changamoto ya nishati katika kanda hiyo.