Featured Kitaifa

SHULE YA SEKONDARI DKT. SAMIA YAGHARIMU BILIONI 17.8

Written by Alex Sonna

 

Na.Alex Sonna-DODOMA

SERIKALI imekabidhiwa rasmi majengo ya Shule ya Sekondari Dkt. Samia iliyopo Iyumbu jijini Dodoma, ambayo imegharimu Shilingi bilioni 17.8. Ujenzi huo, umetekelezwa na Kampuni ya Ujenzi ya Shirika la Uzalishaji Mali Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT CC Limited).

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Septemba 26, 2025 jijini Dodoma, Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Rasilimali Watu katika Wizara hiyo Ndug. Fredrick Kayombo, amesema kuwa amekagua majengo yote na kwamba ameridhishwa na kazi iliyotekelezwa.

‘’Tunaipongeza Serikali chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa katika Shule hii ya mfano, iliyoyosheheni miundombinu bora na kisasa. Ni wajibu wa watendaji kusimamia kikamilifu miundombinu ya shule kwa kuzingatia thamani kubwa ya fedha iliyowekezwa,” Amesema Kayombo.

Amewahimiza wanafunzi wa shule hiyo kusoma kwa bidii ili waweze kufaulu, kuiheshimisha shule yao, na kulinda hadhi yake.

Kwa upande wake Meneja Ujenzi wa Kanda ya Magharibi wa SUMA JKT CC, Kanali Saul Chimwaga amesema ujenzi huo umezingatia viwango vya juu vya ubora, teknolojia na mifumo ya kisasa ikiwemo ya kuzima moto, ulinzi kwa kutumia kamera za CCTV na matumizi ya biogas.

Naye Meneja wa Mradi huo kutoka kampuni ya Ushauri wa Kitaalam Chuo Kikuu Ardhi (ABECC) Dkt. Kimata Malekela, amesema mradi huo unajumuisha jengo la utawala, madarasa, maabara, ofisi za walimu, ofisi, mabweni mawili yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,000 na nyumba 12 za walimu zinazoweza kuchukua walimu 21.

Mkuu wa shule hiyo, Leticia Singo, ameishukuru Serikali kwa kujenga shule bora yenye usajili kamili kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita. Shule hiyo ina wanafunzi 533 wa kidato cha kwanza, tano na sita, na inapokea wanafunzi wa jinsia zote, wakiwemo wenye mahitaji maalum.

Ameeleza kuwa shule hiyo ni jumuishi, ina miundombinu rafiki, mfumo wa biogas kwa shughuli za upishi na uchujaji wa maji taka kwa matumizi ya bustani. Pia imewekewa darasa janja linalowawezesha wanafunzi kujifunza kupitia vituo vilivyounganishwa kitaifa.

About the author

Alex Sonna