MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita serikali imetumia jumla ya Sh bilioni 726 kugawa pembejeo za ruzuku kwa wakulima nchini.
Akihutubia maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Mtwara leo Septemba 26, 2025, wakati akihitimisha mikutano yake ya kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, Dk. Samia amesema kuwa tangu mwaka 2021/22 serikali imekuwa ikitoa pembejeo bure, hususan katika zao la korosho, na kiwango hicho kimekuwa kikiongezeka mwaka hadi mwaka.
“Tunatumia Sh bilioni 192 kila mwaka fedha ambayo ingelipwa na wakulima, lakini sasa tumewaepushia mzigo huo. Mbolea, salfa, dawa za kuua wadudu – vyote vinatolewa bure na serikali kwa lengo la kukuza kilimo na kuongeza uzalishaji wa korosho,” amesema Dk. Samia.
Amebainisha kuwa jitihada hizo zimechangia kuongeza uzalishaji wa zao hilo kutoka tani 118,000 mwaka 2021 zenye thamani ya Sh bilioni 265 hadi kufikia tani 330,505 msimu uliopita, zilizouzwa kwa Sh trilioni 1.9 ambazo zimeingia moja kwa moja kwa wakulima.
Dk. Samia amesisitiza kuwa serikali itaendelea kutoa ruzuku na kuweka mazingira bora ya kilimo, huku akiahidi masoko ya uhakika siyo tu kwa korosho bali pia kwa mazao mengine. “Nchi yetu ni ya pili kwa Afrika kwa uzalishaji wa korosho baada ya Ivory Coast. Tutaendelea kuongeza jitihada ili tuweze kushindana,” amesema
Aidha, ameeleza kuwa jitihada hizo zimeongeza uzalishaji wa mazao mengine kama mbaazi na ufuta sambamba na uwekezaji kwenye skimu za umwagiliaji. “Hapa Mtwara kuna skimu 66, na miradi miwili mikubwa yenye thamani ya Sh bilioni 38.6 inaendelea kujengwa Ndanda (Masasi) na Arusha Chini (Newala),” amesema
Katika sekta ya viwanda, Dk. Samia amesema serikali itaendelea kuvutia uwekezaji katika kongani ya viwanda ya Maranje, wilayani Mtwara. Pia aliahidi kuimarisha vyama vya ushirika kwa kuhakikisha vinajitegemea na vinatoa huduma bora bila ubadhirifu wala ucheleweshaji wa malipo kwa wakulima.
Ametaja hatua zilizochukuliwa, alisema serikali tayari imeanzisha benki ya ushirika mahsusi kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa vyama vya ushirika nchini.