Featured Kitaifa

DC MAYANJA:TANZANIA ITAJENGWA NA WATANZANIA WENYEWE

Written by Alex Sonna

 

 

Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Janeth Mayanja,akizungumza leo Septemba  26.09.2025 na timu ya maafisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) walipofika ofisini kwake kwa ajili ya kujitambulisha na kumtaarifu juu ya zoezi la kampeni ya elimu ya kodi mlango mlango wilayani humo.

Na.Yahya Saleh-Chamwino

“Hatuna nchi nyingine zaidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na nchi hii itajengwa na Watanzania wenyewe.”

Ni kauli ya Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma Mhe. Janeth Mayanja wakati akizungumza leo Ijumaa tarehe 26.09.2025 na timu ya maafisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) walipofika ofisini kwake kwa ajili ya kujitambulisha na kumtaarifu juu ya zoezi la kampeni ya elimu ya kodi mlango mlango wilayani humo.

Mhe. Mayanja amesema kuwa, nchi inajengwa kutokana na kodi zinazolipwa na wananchi.

“Miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa hapa nchini, inatokana na kodi za watanzania hivyo ni wajibu wa kila mtu mwenye vigezo vya kulipa kodi, alipe kodi kwa wakati,” alieleza Mhe. Mayanja.

Aidha, ameipongeza TRA kwa kuendelea kukusanya kodi kwa weledi na kuvuka malengo ya makusanyo huku akiisisitiza TRA kuhakikisha kila kodi inayotakiwa kukusanywa ikusanywe kwa Maendeleo ya Taifa.

“Naomba muendelee kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato na mjitahidi kuwafikia walipakodi walioko kwenye kata na vijiji mbalimbali ili sote kwa pamoja tuchangie maendeleo ya nchi yetu,” alisistiza Mkuu huyo wa Wilaya.

Naye Meneja wa TRA Wilayani Chamwino Bi. Ester Mallya amesema kuwa, kwa sasa wamejipanga kuongeza ushirikiano baina yao na Watendaji wa Kata na Wenyeviti wa Mitaa ili kuhakikisha elimu ya kodi inawafikia watu wote pamoja na kuwasajili wale wanaostahili kusajiliwa.

About the author

Alex Sonna