Na Gideon Gregory, Dodoma
Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) imempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na serikali yake kwa hatua kubwa ya kupunguza kero za kodi na ushuru kwa zaidi ya asilimia 85, hali ambayo imeleta nafuu katika biashara na kuongeza makusanyo ya mapato.
Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Mtendaji wa jumuiya hiyo, Alexander Mallya leo Septemba 17,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuongeza kuwa kwasasa wafanyabiashara wanafanya kazi katika mazingira bora zaidi, tofauti na zamani ambapo changamoto za kodi zilikuwa kikwazo kikubwa.
“Jumla ya kero 119 zilizowasilishwa na wafanyabiashara, 109 zimepatiwa ufumbuzi na kubaki kero 18 pekee, huku 36 zikiwa katika hatua za mwisho za kumaliziwa hii ni hatua kubwa ambayo Serikali yetu imetufanyia hivyo hatuna budi kutoa pongezi zetu kwa serikali, “amesema.
Kwa mujibu wa Mallya, hatua hiyo ni ushahidi wa dhamira ya Rais Samia katika kujenga mazingira rafiki ya biashara na kuondoa urasimu uliokuwa unadumaza sekta hiyo.
Aidha, Mallya amesema wafanyabiashara wanatamani kushiriki kikamilifu kwenye sekta za kimkakati kama kilimo, madini na viwanda ili kuchochea ukuaji wa uchumi.
Mbali na hilo, amefafanua kuwa miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa Dodoma ikiwemo reli ya kisasa ya SGR, Magufuli City, na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato imefungua fursa kubwa za biashara, ajira na usafirishaji wa bidhaa.
Kwa upande wa mapato, amesema Dodoma imefanikiwa kuvuka lengo la makusanyo ya kodi baada ya kufikia zaidi ya shilingi bilioni 204 dhidi ya lengo la awali la shilingi bilioni 88 pekee.
“Mafanikio haya yanaonyesha uaminifu wa wafanyabiashara kulipa kodi na mchango mkubwa wa serikali katika kurahisisha mifumo ya ukusanyaji kodi ikiwa ni hatua ya kuendelea kukuza pato la nchi, “amesema.
Mallya pia amesisitiza kuwa serikali haiwezi kumtoza kodi kubwa mfanyabiashara mdogo, badala yake kila mmoja analipa kulingana na ukubwa wa biashara yake.
Ameeleza kuwa ulipaji wa kodi kwa hiari ndio msingi wa kujenga shule, hospitali, barabara na huduma nyingine za kijamii zinazowanufaisha wananchi wote.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Dodoma, Gilbert Chuwa, amepongeza serikali kwa kuondoa urasimu uliokuwa unaleta uadui kati ya wafanyabiashara na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Naye mfanyabiashara Sylivano James Chami amesema tofauti na zamani ambapo baadhi ya wafanyabiashara walilazimika kufunga maduka kutokana na madeni na changamoto za kodi, sasa mazingira yamekuwa salama na rafiki, hivyo akawataka wenzao kulipa kodi kwa hiari na kuunga mkono jitihada za serikali ya Rais Samia.