Featured Michezo

MICHEZO IWE SILAHA MPYA DHIDI YA UHALIFU KATIKA JAMII.

Written by Alex Sonna

Na Issa Mwadangala.

Wanamichezo, wadau wa michezo, mashabiki na wananchi wa Kitongoji cha Hazuru B Kata ya Hasamba Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe wametakiwa kuuchukia uhalifu ikiwa ni pamoja na kuwa walinzi wa haki za binadamu, amani na usalama wa jamii yao.

Hayo yameelezwa Septemba 14, 2025 na Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Maria Kway katika fainali ya michuano ya Mavuno Cup ambapo timu kongwe za Majimaji FC na Sumaila FC zilipambana vikali, huku akitoa elimu kwa kina kuhusu ukatili wa kijinsia na madhara yake, alieleza kuwa ukatili huo unawaathiri watoto, wanawake, na hata wanaume, na kuhimiza jamii kutofumbia macho vitendo hivyo, bali watoe taarifa kwa Jeshi la Polisi mapema ili hatua  zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.

Vilevile, ACP Kway alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani kuelekea Uchaguzi Mkuu, akiwataka wananchi hao kuwa makini na vikundi vya uchochezi na kuhimiza mshikamano wakati na baada ya uchaguzi ili Songwe iendelee kuwa salama.

Aidha, ACP Kway, alitoa elimu kwa kinagaubaga kuhusu kampeni ya kitaifa ya usalimishaji wa silaha haramu, huku akibainisha kuwa kampeni hiyo ilianza rasmi Septemba 01 hadi 30 Oktoba, na kuwataka wananchi wanaomiliki silaha kinyume cha sheria wanatakiwa kuzikabidhi kwa hiari bila kufunguliwa mashtaka kabla ya muda wa msamaha kumalizika.

Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Mbozi Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Deborah Mhekwa, aliwataka wananchi hao kuongeza juhudi za kukomesha mimba za utotoni, kwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi, huku akiwasisitiza kuwa mimba za utotoni hukatisha ndoto za watoto wa kike na kuongeza utegemezi katika jamii, hivyo aliwataka wazazi, walezi na jamii nzima kushirikiana katika malezi bora ili watoto wa kike waweze kutimiza ndoto zao za baadae.

Ikumbukwe kuwa fainali ya Mavuno Cup ndani ya Kata ya Hasamba imeendelea kuonyesha wazi kuwa michezo ni zaidi ya burudani, pia ni jukwaa la kukuza uelewa wa haki za binadamu, ustawi wa jamii, na ujenzi wa taifa lenye amani na mshikamano.
WhatsApp Image 2025-09-14 at 21.52.38_73faff53.jpg
ACP MARIA KWAY AKIONGEA NA WANANICHI HAO.
WhatsApp Image 2025-09-14 at 21.52.38_2817d046.jpg
ASP DEBORAH MHEKWA AKIONGEA NA WANANCHI HAO.
WhatsApp Image 2025-09-14 at 21.52.39_9f4daa9b.jpg

WhatsApp Image 2025-09-14 at 21.52.39_6f2cf016.jpg
ACP KWAY NA ASP MHEKWA WAKIWA KWENYE PICHA YA PAMOJA NA WACHEZAJI WA MAJIMAJI FC.

About the author

Alex Sonna