Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia, Badru Abdunuru,akizungumza wakati akifunga mafunzo ya Ujumuishaji wa bajeti kwa maafisa wa Serikali kutoka Wizara mbalimbali kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu,leo Septemba 3,2025 jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo, taasisi na sekta binafsi kuhakikisha masuala ya usawa wa kijinsia yanapewa kipaumbele katika sera, mipango na bajeti.
Hayo yamesemwa leo Septemba 3, 2025 Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia, Badru Abdunuru kwa niaba ya Dkt. John Jingu, wakati akifunga mafunzo ya Ujumuishaji wa bajeti kwa maafisa wa Serikali kutoka Wizara mbalimbali.
Bw.Badru amesema kuwa ushirikiano huo umekuwa chachu ya mafanikio katika sekta mbalimbali.
Kwa upande wake Mwalilishi kutoka Umoja wa Ulaya (EU) Alexandra Pissat amesema ili kuleta usawa wa kijinsia ni muhimu kuzingatia bajeti katika masuala ya jinsia, kufanya tathmini na ufuatiliaji ili kuendelea kuondoka changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kurudisha nyumba mipango ya kuleta usawa wa kijinsia nchini.
“Mabadiliko chanya na maendeleo kwa jamii yanapatikana tu ikiwa usawa wa kijinsia unazingatiwa katika mipango ya Serikali katika utekelelezaji wa ajenda mbalimbali za kuwawezesha wanawake katika masuala ya jinsia.” amesisitiza Alexandra
Naye Mwakilishi kutoka Wizara ya Maji, Susan Magoli amesema mafunzo hayo yamekuwa msaada mkubwa kwani yanaelekeza kutoa kipaumbele katika kutenga bajeti kwa kuhusisha masuala ya usawa wa kijinsia jambo ambalo litachangia maendeleo na ushiriki wa wanawake katika uwezeshaji na uongozi.
Mafunzo hayo yalishirikisha washiriki zaidi ya 200 kutoka Wizara na Wakala za Serikali yakiandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU), yakilenga kutoa elimu ya ujumuishaji wa masuala ya jinsia katika bajeti ili kuleta usawa wa kijinsia, kuongeza uelewa na kuwapa washiriki zana, maarifa na ujuzi unaohitajika ili kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake katika mipango na bajeti za Wizara za kisekta, kwa kuzingatia Sera ya Jinsia 2023 na Dira ya 2050.