Featured Kitaifa

AZZA HILLAL HAMAD AONGOZA KURA ZA MAONI JIMBO JIPYA LA ITWANGI

Written by Alex Sonna
Azza Hilal Hamad
Azza Hilal Hamad

Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mbunge wa zamani wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga, Azza Hillal Hamad, ameongoza katika kura za maoni za CCM Wilaya ya Shinyanga Vijijini, kwa nafasi ya ubunge wa Jimbo Jipya la Itwangi, akipata kura 2,630 kati ya kura 5,580 zilizopigwa.

 Kura halali  zilikuwa 5551 na kura  zilizoharibika  ni 29.

Azza Hillal ambaye amewahi kulitumikia Bunge kwa kipindi cha miaka 10 kupitia nafasi ya Viti Maalum, alikuwa anachuana vikali na wagombea wengine saba akiwemo John Elias Ntalimbo aliyeshika nafasi ya pili kwa kupata kura 2,322. Wagombea wengine waliopata kura ni: Sebastian Pastory Malunde (kura 377), Fred Romanus Sanga (kura 122), Chrispine Myeke Simon (kura 45), Christian Misobi Budoya (kura 28), Anna James Ng’wagi (kura 16), na Hellena Daudi Mbuli aliyepata kura 11.

Akitangaza matokeo hayo, Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Vijijini na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Erenestina Richard, amesema kuwa matokeo haya ni ya awali, na uteuzi wa mwisho wa mgombea wa CCM utafanywa na vikao vya juu vya chama.

“Kuongoza katika kura za maoni siyo ushindi wala siyo kuwa umeteuliwa kuwa mgombea.Tunawaomba wagombea wote wawe watulivu na wasubiri kwa subira maamuzi ya vikao vya uteuzi vya chama,” amesema.

Jimbo la Itwangi ni miongoni mwa majimbo mapya yaliyoundwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, likiwa limezua mvuto mkubwa kwa wananchi, wanachama na wapiga kura wa CCM katika mkoa wa Shinyanga.

About the author

Alex Sonna