Ahmed Ally Salum
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Mbunge aliyemaliza muda wake, Ahmed Ally Salum, ameongoza kwa kishindo katika kura za maoni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Vijijini, kwa nafasi ya ubunge wa Jimbo la Solwa, akijizolea kura 3,862 kati ya kura 7012 zilizopigwa na hakuna kura iliyoharibika.
Ahmed Salum alikuwa anachuana na wagombea wengine sita akiwemo Sosthenes Julius Katwale aliyeshika nafasi ya pili kwa kupata kura 2,288, akifuatiwa na Selemani Emmanuel Chokala (kura 645), Zinguji Mayala Machwele (kura 67), Alphistone Michael Bushi (kura 61), Costantine Joseph Budaga (kura 59) na Leonard Nduta Lukanya aliyepata kura 30.
Akizungumza baada ya kutangaza matokeo hayo, Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Vijijini ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi, Erenestina Richard, amesema kuwa matokeo hayo ni ya awali, na uteuzi rasmi wa mgombea wa CCM bado unasubiriwa kupitia vikao vya juu vya uteuzi vya chama.
“Kuongoza katika kura za maoni siyo ushindi wala siyo kuwa umeteuliwa kuwa mgombea. Tunawaomba wagombea wote wawe watulivu na kusubiri maamuzi ya vikao vya uteuzi vya chama,” amesema.