Featured Kitaifa

WATENDAJI WA UCHAGUZI WATAKIWA KUSOMA KUSOMA KATIBA, SHERIA, KANUNI ZA TUME

Written by mzalendoeditor

Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Sheria wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Cyprian Mbugano, akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya siku tatu kwa watendaji wa Uchaguzi kutoka mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida. 

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka Waratibu wa Uchaguzi wa Mikoa ,Wasimamizi wa Uchaguzi,Wasimamizi wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maofisa uchaguzi na maofisa ununuzi kutenga sehemu ya muda wao kusoma Katiba, sheria na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Tume hiyo.
 
Lengo  la kusoma Katiba,sheria na maelekezo mbalimbali  yanayotolewa na Tume hiyo  ili yawaongoze katika kusimamia vyema uchaguzi utakaokuwa huru na haki.
 
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Sheria wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Cyprian Mbugano, alisema hayo  jana kwa niaba ya  Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufaa, Jacobs wakati wa ufungaji  wa mafunzo  ya siku tatu kwa wasimamizi hao wapatao 165 kutoka halamshauri 24 za mikoa ya Dodoma , Singida na Morogoro.
 
Katika mafunzo hayo mada 12 ziliwasilishwa kwa washiriki kujifunza , na  kauli mbiu ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2025 ni ‘ Kura yako, Haki yako, Jitokeze kupiga kura”.
 
“ Kama ilivyoelezwa wakati wa ufunguzi wa mafunzo haya , shughuli zote za uchaguzi zinaongozwa na Katiba , sheria , kanuni , maadili ya uchaguzi na maelekezo ya Tume hivyo mkikutana na changamoto zozote msisite kufanya mawasilino na watendaji wa Tume ” alisema Mbugano .
 
“ Jukumu lililo mbele yenu ni kubwa na muhimu, linaahitaji umakini na kujitoa , hivyo ni matarajio ya Tume kwamba , baada ya kupatiwa mafunzo haya , mtatekeleza majukumu yenu kwa ufanisi na weledi mkizingatia ratiba ya utekelezaji ili kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba Mwaka 2025 unaotarajiwa” alisisitiza Mbugano.
 
Kwa upande wa ajira za kupata watendaji wa vituo, alisema kuwa Tume inayoimani ya kwamba watateua na kuajiri watendaji wenye sifa na uwezo wa kufanya kazi hiyo muhimu  , jambo ambalo limekuwa likisisitizwa tangu mwanzo wa mafunzo hayo.
 
“ Watendaji hawa wa vituo ndio watakaosimamia zoezi la kupinga kura na kuhesabu kura vituoni , kazi ambayo inahitaji umahiri , umakini na weledi katika kuitekeleza” alisisitiza Mbugano.
 
Alisema ni imani ya Tume kuwa mafunzo ya watendaji wa vituo yatafanyika kwa ufanisi na weledi katika tarehe zilizopangwa kwenye ratiba ya utekelezaji wa shughuli za uchaguzi na yanalenga kuwajengea uwezo ili waweze kufahamu majukumu  yao na kuyatekeleza ipasavyo wakati wa uchaguzi.
 
Mbugano alitumia nafasi hiyo kuwaasa wasimamizi hao kubandika matangazo mbalimbali ya kisheria kuhusiana na uchaguzi pamoja na mabango mbalimbali yanayotakiwa kwa mujibu wa maelekezo .
 
Alisema ikumbukwe kuwa ,wapo wadau mbalimbali wa uchaguzi kama vile waangalizi wa uchaguzi kutoka ndani na n je ya nchi ambao wanafuatilia uendeshwaji wa uchaguzi na kiwango cha kuzingatiwaji wa sheria zinazohusiana na uchaguzi , hivyo wahakikishe wanazigatia  maelekezo yanayotolewa na Tume kila wakati.
 
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake, Mwenyekiti wa Mafunzo hayo, Dismass Pesambili aliishukuru Serikali kupitia Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kuwawezesha mafunzo hayo ambayo ni silaha na nyenzo muhimu ya kufanikisha uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu .

About the author

mzalendoeditor