Na Angela Msimbira, Seoul, Korea
Serikali ya Korea Kusini kupitia shirika la KOICA imeandaa Mkutano wa Kimataifa kubadilishana uzoefu kwenye kuboresha mifumo ya usimamizi wa huduma za afya kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Mkutano huu umehusisha watalaam kutoka Tanzania na Korea ikiwa ni sehemu ya ushirikiano wa Mradi wa Kupanua matumizi ya Mfumo wa GOTHOMIS unaotelekelezwa Mkoani Dodoma.
Akizungumza kwa niaba ya ujumbe wa Tanzania, Mkurugenzi Msaidizi – (Huduma za Lishe) Bw. Lutifrid Nnally, amesema ushiriki wa Tanzania unalenga kujifunza uzoefu wa Korea kwenye matumizi ya mifumo ya kidijitali katika huduma za afya.
Tanzania inatarajia kutumia uzoefu huo kufanya maboresho ya GOTHOMIS, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa kutumia teknolojia kama telemedicine, akili bandia (AI) na mifumo ya taarifa za kiafya.
Ushiriki huu ni hatua muhimu katika mageuzi ya sekta ya afya, hasa kwa maeneo ya vijijini, ili kuhakikisha huduma bora, za haraka na kwa gharama nafuu zinawafikia wananchi wote.