Featured Kitaifa

BUNGE LAPITISHA KWA KISHINDO BAJETI YA SERIKALI MWAKA 2025/26 YA SH. TRILIONI 56.49

Written by mzalendoeditor

 

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akijibu hoja mbalimbali za wabunge wa kuhitimisha Mapendekezo ya Serikali ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2025/26, bungeni jijini Dodoma

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akijibu hoja mbalimbali za wabunge wa kuhitimisha Mapendekezo ya Serikali ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2025/26, bungeni jijini Dodoma

Wabunge mbalimbali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiwapongeza Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Naibu wake, Mhe. Hamad Hassan Chande, baada ya wabunge hao kupitisha kwa kishindo makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali ya Shilingi Trilioni 56.49 kwa mwaka 2025/26, ambapo zaidi ya wabunge 373 sawa na Asilimia 98.7 walipitisha kwa kura ya ndio.
 
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)
Na. Joseph Mahumi, WF, Dodoma
 
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limepitisha kwa kishindo makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali ya shilingi trilioni 56.49 kwa mwaka wa Fedha 2025/26, ambapo zaidi ya wabunge 373 sawa na Asilimia 98.7 walipitisha kwa kura ya ndiyo.
 
Akizungumza wakati akifafanua maswali mbalimbali ya wabunge kabla ya zoezi la upigaji  kura ya wazi ya kupitisha Bajeti hiyo, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alisema kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha kupitia Bajeti hiyo ya 2025/26, malengo ya ukuaji wa uchumi yatafikiwa kwa kuzingatia utekelezaji madhubuti wa miradi ya maendeleo kama ilivyoainishwa katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo (FYDP III) ikiwemo miradi ya kielelezo na kimkakati; kuendelea kuimarisha miradi ya uzalishaji; na kuimarisha ubora wa rasilimali watu hususan katika sekta za huduma za jamii.
 
“Serikali itaendelea kudhibiti mfumuko wa bei nchini ili kukabiliana na mabadiliko ya bei za bidhaa duniani kwa kuimarisha sekta mbalimbali za uzalishaji ikiwa ni pamoja na: kuongeza matumizi ya gesi asilia inayozalishwa nchini pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza uagizaji wa bidhaa za petroli kutoka nje ya nchi; kuboresha mazingira ili kuchochea uzalishaji wa mbolea, mafuta ya kula, sukari na bidhaa nyingine muhimu ili kupunguza uagizaji wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi; kuendelea na utekelezaji wa sera madhubuti za fedha na za bajeti; na kuongeza uzalishaji wa mazao ili kuwezesha upatikanaji wa chakula katika masoko ya ndani” alisema Mhe. Dkt. Nchemba.
 
Aidha,  Mhe. Dkt. Nchemba alisema kuwa, kwa kutambua umuhimu wa Sekta za Uzalishaji katika kukuza Pato la Taifa, kuchachua uchumi na kutoa ajira kwa wananchi kiasi cha shilingi trilioni 10.24 kimetengwa kwa ajili ya sekta hizo, sawa na asilimia 18.12 ya bajeti ya Serikali ya mwaka 2025/26.
 
“Bajeti hii imezingatia utekelezaji wa vipaumbele vingine ikiwemo ujenzi na ukarabati wa viwanja mbalimbali kwa ajili ya maandalizi ya AFCON 2027, maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 pamoja na ukamilishaji wa miradi ya kielelezo na kimkakati” alisema Dkt. Nchemba.
 
Mhe. Dkt. Nchemba aliongeza kuwa, Serikali kwa kutambua umuhimu wa sekta ya kilimo, kwa mwaka 2025/26, Serikali imetenga jumla ya shilingi trilioni 1.9 kwa ajili ya sekta ya kilimo sawa na ongezeko la asilimia 203.6 kutoka bajeti ya mwaka 2021/22.
 
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwashukuru wabunge wote waliochangia bajeti ya Serikali 2025/26 kwa kuzungumza na kwa maandishi.
 
“Hakika tunathamini michango yote iliyotolewa kutokana na tija yake katika kujenga uelewa wa pamoja na kutanguliza vipaumbele vya wananchi tunaowawakilisha kwa maslahi mapana ya Taifa letu. Kitu kimoja ambacho ni dhahiri kama walivyochangia waheshimiwa wabunge ni kuwa hatuna deni na MAMA hasa baada ya kukamilisha yale yote yaliyoabainishwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020” alisema Dkt. Nchemba
 
Alitamatisha akisema kuwa Bunge la 12 limeweka alama kubwa kwa nchi kwa kupitisha sheria, maazimio na mipango mbalimbali yenye manufaa kwa wananchi. 
 
“Waheshimiwa Wabunge mtakumbukwa sana kwa kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kusukuma gurudumu la maendeleo kwa nchi yetu hususan kupitia utekelezaji wa miradi yenye matokeo chanya katika sekta mbalimbali za kiuchumi ikiwemo sekta za uzalishaji, miundombinu wezeshi pamoja na huduma za kijamii” alisema Dkt. Nchemba 
 
Bajeti ya Serikali 2025/26 inatarajiwa kugharamiwa na mapato ya ndani ya shilingi trilioni 40.47, misaada shilingi trilioni 1.07 na mikopo ya shilingi trilioni 14.95. Kati ya mapato ya ndani yanayotarajiwa, mapato ya kodi ni shilingi trilioni 32.31, mapato yasiyo ya kodi shilingi trilioni 6.48, na mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa shilingi trilioni 1.68. Aidha, mikopo inajumuisha shilingi trilioni 6.27 kutoka vyanzo vya ndani na shilingi trilioni 8.68 kutoka vyanzo vya nje. 
 
Aidha,makadirio ya matumizi ya Serikali ya shilingi trilioni 56.49 kwa mwaka 2025/26 yanajumuisha: Stahiki za watumishi na michango ya pensheni (Serikali Kuu) shilingi trilioni 7.71; ununuzi wa bidhaa na huduma shilingi trilioni 7.81; malipo ya riba za mikopo shilingi trilioni 6.49; na ruzuku (subsidies & transfers) kwa taasisi za Serikali, mashirika ya umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa shilingi trilioni 23.04. Aidha, Serikali inatarajia kutumia shilingi trilioni 7.72 kugharamia malipo ya mtaji kwa deni la ndani na nje.

About the author

mzalendoeditor