Featured Kitaifa

THBUB YAHIMIZA WANANCHI NA WATUMISHI KUHESHIMU MISINGI YA UTAWALA BORA

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imetoa wito kwa Wananchi na watumishi wa umma nchini kuhakikisha kuwa wanazingatia misingi ya utawala bora katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Wito huo umetolewa na Mchunguzi Msaidizi Mkuu Bw. Paul Sulle alipokuwa akitoa elimu ya haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa watumishi na wananchi waliotembelea banda la THBUB lililopo katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Viwanja vya Chinangali Park Jijini Dodoma.

Bw. Sulle amesisitiza kuwa kutenda kazi kwa uwazi, uwajibikaji, uadilifu, usawa na kuheshimu haki za binadamu ni nguzo muhimu katika kutoa huduma kwa wananchi.

“Watumishi wa Umma wanapaswa kutambua kwamba Misingi ya utawala bora si chaguo bali ni wajibu wa kisheria na kikatiba. Wanatakiwa kutoa huduma kwa haki bila upendeleo, pamoja na kushughulikia kero za wananchi kwa wakati,”amesema Bw. Sulle.

Aidha, ameeleza kuwa ucheleweshaji wa huduma, matumizi mabaya ya madaraka, ukosefu wa taarifa kwa umma, na kukosa uwajibikaji ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora na huathiri ustawi wa wananchi na kuvunja imani yao kwa baadhi ya taasisi za serikali.

About the author

mzalendo