Featured Kitaifa

LESENI ZA MADINI SASA KUTOLEWA KWA UWAZI NA UFANISI ZAIDI

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu, Dodoma 

Afisa Elimu, Kazi na Jinsia kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), Bwana Nsubisi Mwasandende, ameipongeza Tume ya Madini kwa juhudi kubwa inazozifanya katika kusimamia rasilimali za madini nchini na kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa.

Akizungumza katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma, Mwasandende amesema kuwa mchango wa Sekta ya Madini kwenye uchumi wa nchi umeendelea kuongezeka kwa kasi.

“Ripoti za hivi karibuni zinaonyesha kuwa Sekta ya Madini imechangia zaidi ya asilimia 10 ya Pato la Taifa (GDP). Hili ni jambo la kujivunia na nawapongeza sana Tume ya Madini kwa kazi nzuri wanayoifanya, amesema.

Kwa upande wake, Mhandisi wa Migodi, Bi. Colliness Seiya, ameeleza kuwa Tume ya Madini imefanya maboresho makubwa kwenye mfumo wa utoaji wa leseni kwa lengo la kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi wa shughuli za uchimbaji wa madini.

“Mfumo wa sasa wa utoaji wa leseni umejengwa kidijitali kupitia Online Mining Cadastre Transactional Portal (OMCTP), ambapo waombaji wanatuma maombi yao mtandaoni. Hii imepunguza urasimu na kutoa nafasi kwa uwazi zaidi katika mchakato wa maombi,” amesema Mhandisi Colliness.

Aidha, ameeleza kuwa mfumo huo unawawezesha waombaji wa leseni za utafutaji au uchimbaji wa madini kufuatilia hatua zote za maombi yao kwa njia ya mtandao bila ya kulazimika kufika katika ofisi za serikali.

“Hii imeongeza ufanisi na kupunguza malalamiko ya upendeleo. Kila hatua inaonekana wazi na kwa wakati,” ameongeza.

Kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na marekebisho yake, Tume ya Madini inatoa aina mbalimbali za leseni kulingana na shughuli husika, ikiwemo:
_• Leseni ya Utafutaji wa Madini (Prospecting Licence)_
_• Leseni ya Uchimbaji Mdogo (Primary Mining Licence)_
_• Leseni ya Uchimbaji wa Kati na Mkubwa (Mining Licence na Special Mining Licence)_

Mhandisi Colliness amebainisha kuwa kumekuwa na ongezeko la maombi ya leseni kutokana na kuongezeka kwa uelewa miongoni mwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuendesha shughuli za madini kwa kuzingatia sheria na taratibu.

Aidha, utoaji wa leseni kwa uwazi umewezesha ukusanyaji madhubuti wa mapato ya Serikali kupitia ada na tozo mbalimbali, utunzaji wa mazingira na usimamizi wa haki za jamii katika maeneo ya uchimbaji.

“Mfumo huu si tu umesaidia kuongeza mapato ya Serikali, bali pia umekuwa chombo muhimu cha kuhakikisha mazingira na jamii zinazozunguka maeneo ya madini zinalindwa ipasavyo,” amehitimisha.

About the author

mzalendo