Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Uhusishwaji kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mha. Charles Nyange amesema mikoa inayoshika kasi kwenye matumizi ya nishati ya gesi ni pamoja na Mtwara, Lindi na Dar es Salaam.
Akizungumza leo Juni 17,2025 Jijini Dodoma katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Mha. Nyange amesema uwekezaji katika gesi asilia katika maeneo hayo unaendelea kukua kwa kasi hivyo kuchagiza katika hatua hiyo.
“Kutokana na umuhimu wa gesi asilia hasa kwa matumizi ya majumbani, PURA inaendelea na juhudi za kusambaza miundombinu ya gesi hiyo kadri rasilimali fedha zinavyopatikana,” amesema.
Mha. Nyange amesema kuwa tayari baadhi ya Watanzania wamenufaika kupitia ajira za muda na ajira za kudumu zinazotokana na shughuli za gesi asilia, hatua inayosaidia kuinua kipato cha wananchi na kuchochea maendeleo ya ndani.
Aidha, PURA inalenga kuwajengea uwezo Watanzania na kampuni za ndani ili washiriki kikamilifu katika miradi ya utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini.
“Malengo yetu mengine ni kuhamasisha uwekezaji zaidi katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia, kuwafikia wananchi kwa awamu na kukuza fursa za ajira,” amesema Mhandisi Nyange.
Ameongeza kuwa PURA imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha rasilimali za mafuta na gesi zinatumika kwa manufaa ya Taifa na kuwanufaisha Watanzania kupitia ushiriki wa moja kwa moja na wa kimkakati katika sekta hiyo muhimu.