Featured Kitaifa

SERIKALI KUNUNIA TANI LAKI 2 ZA MBOLEA VIWANDA VYA NDANI.

Written by mzalendoeditor

WAZIRI  wa Kilimo Mhe.Hussein Bashe, akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 11,2025 jijini Dodoma kuelekea katika uzinduzi wa kiwanda  cha uzalishaji wa Mbolea cha ITRACOM Fertilizers Ltd  kilichopo  Nala, jijini Dodoma.

WAZIRI  wa Kilimo Mhe.Hussein Bashe, akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 11,2025 jijini Dodoma kuelekea katika uzinduzi wa kiwanda  cha uzalishaji wa Mbolea cha ITRACOM Fertilizers Ltd  kilichopo  Nala, jijini Dodoma.

Na.Alex Sonna-DODOMA

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan,anatarajiwa kuzindua kiwanda cha uzalishaji wa Mbolea cha ITRACOM Fertilizers Ltd  kilichopo  Nala, jijini Dodoma pamoja na kuweka  jiwe la msingi, kupanda miti kama ishara ya kukuza  mazingira na kilimo endelevu, kukagua miundombinu ya kisasa ya  Kiwanda hicho.

Hayo yameelezwa leo Juni 11,2025 na Waziri wa Kilimo Mhe.Hussein Bashe,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea katika uzinduzi wa kiwanda hicho utakaofanyika Juni 28 mwaka huu ambapo Kauli mbiu ya hafla hiyo ni “Kilimo  ni Mbolea na Mbolea ni FOMI”. 

Amesema kuwa Kiwanda  hicho kimeweza kuajiri  watumishi wapatao 1805. Ajira  zisizokuwa za moja kwa moja zinazotokana na kiwanda  kuwepo zinakadiriwa kuwa zaidi ya 5,000. Kiwanda kinatazamia  kuajiri watu zaidi ya 3,000 na kuwa na ajira zisizokuwa za moja kwa  moja zaidi ya 15,000.  

‘Ujenzi wa Kiwanda hicho  ulianza mwaka 2021 ambapo kina uwezo wa  kutengeneza aina mbalimbali za mbolea kutegemeana na aina za  udongo na mazao. Kwa sasa kimeshasajili aina 14 za mbolea,  zinazotumika kwa mazao yote yanayolimwa Tanzania. Kiwanda pia  kinazalisha chokaa-kilimo kwa ajili udongo ulioathirika na tindikali. “amesema Mhe.Bashe

Aidha amesema kuwa Mbolea aina za Fomi Otesha, Fomi Kuzia na Fomi Nenepesha zilianza  kuingia sokoni Mwezi Desemba 2022 ambazo hutumika kuboresha  afya ya udongo na kuongeza mavuno kwenye mazao ya chakula na  biashara.  

Hata hivyo Waziri Bashe amesema kuwa  katika kuhakikisha wanalinda viwanda vya ndani Serikali imejipanga kununua mbolea tani laki 2 katika viwanda vya ndani na tani elfu 50 za chokaa kwaajili ya kuboresha shughuli za kilimo.
Amesema ununuzi huo wa Mbolea hautalenga  kuathiri mfumo wa ruzuku unaoendelea kwani wao watapeleka zaidi maeneo yale ambayo mbolea hazitumiki kwa wingi ili Watanzania wahamasike kuzitumia na kuona matokeo.
“Ili kulinda viwanda vyetu vya ndani Serikali mwaka huu imeamua itanunua mbolea kutoka viwanda vya ndani tani laki 2 na tani elfu 50 zitanunuliwa nu za chokaa kwaajili ya shughuli za kilimo”.
“Na pia Serikali itanunua hizi mbolea bila kuathiri mfumo wa ruzuku unaoendelea, ila zitakaponunuliwa tutazipeleka kwenye maeneo ambayo mbolea hazitumiki sana ili Watanzania waanze kutumia za viwanda vya ndani na kuona matoke yake”.amesema
Aidha amesema Nchi imekuwa ikiagiza karibu tani milioni 1.2 za mbolea kutoka nje lakini kwasasa kutokana na uwepo wa kiwanda hiki na uwekezaji wake mahitaji ya mbolea yatapatikana kutoka viwanda vya ndani.
Pia Waziri Bashe ametoa hamasa kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma  na Mikao ya Jirani kujitokeza kwa wingi ili kushiriki katika uzinduzi huo  wa kihistoria.  
Naye Mkurugenzi wa Kiwanda cha Itracom Fertilisers Limited Bwana Nduwimana Nazaire amesema kuwa wao kwa kushirikiana na Taasisi za Serikali kama vile TARI na TFRA mpaka sasa tayari kuna aina 14 ambazo kiwanda kinazalisha ambapo pia kiwanda kina uwezo wa kutengeneza mbolea kulingana na eneo,kulingana na zao na pia kulingana na hitaji la mkulima.
Na kuongeza kuwa kiwanda hicho  kinazalisha mbolea mchanganyiko  wa chumvi chumvi na malighafi za asili kama vile samadi na zinginezo.
Uzinduzi huu ni miaka mitatu na nusu toka uwekezaji huu kuanza kufanyika hapa Jijini Dodoma.

Uzinduzi huo pia utahudhuriwa na Waheshimiwa Marais wa nchi jirani  akiwemo Mhe. Meja Jenerali (Mst) Evariste Ndayishimiye, Rais wa  Jamhuri ya Burundi; na Viongozi Wakuu wa Serikali wakiwemo  Mawaziri wa Kilimo kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa  Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiongozwa na Waziri wa Kilimo  wa Tanzania, Mhe. Hussein Bashe (Mb); Makatibu Wakuu; Wakuu wa  Mikoa; Wakuu wa Wilaya na Wananchi wa Dodoma na mikoa ya jirani.

About the author

mzalendoeditor