Featured Kitaifa

BAJETI KUU YA SERIKALI, BAJETI KUU YA SERIKALI, WANANCHI WAHIMIZWA KUIFUATILIA

Written by mzalendoeditor

Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa,akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 11,2025 katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.

Na.Meleka Kulwa-DODOMA

Wizara ya Fedha na Wizara ya Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji inatarajiwa kuwasilisha bajeti kuu ya serikali pamoja na hali ya uchumi kwa mara ya kwanza, ikiwa bajeti hiyo inahudumiwa kwa fedha za ndani.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma Leo tarehe 11 juni 2025 Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, bajeti hii ni ya kihistoria kwa sababu itatoa mwelekeo wa bajeti ya uchaguzi wa mwaka 2025.

Msigwa alitoa wito kwa wananchi kufuatilia kwa karibu bajeti hiyo, akisisitiza kuwa ni fursa ya kuona maendeleo makubwa yaliyofikiwa chini ya serikali ya Awamu ya Sita. “Hii ni bajeti ya mwisho ya serikali ya Awamu ya Sita na itakuwa ya kipekee kwa sababu asilimia kubwa ya fedha zinatokana na mapato ya ndani,” alisema Msigwa.

GAWIO LA MASHIRIKA YA UMMA

Tanzania imeandika historia kwa kupokea gawio la shilingi trilioni 1.28 kutoka mashirika ya umma, hatua inayotokana na jitihada za serikali ya Awamu ya Sita kuongeza uwekezaji hadi kufikia shilingi trilioni 86. Msigwa alisema kuwa mafanikio haya yamechagizwa na utekelezaji wa 4R zilizoasisiwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Alisisitiza kuwa gawio hilo litakuwa likiongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na uwekezaji wa kina uliofanyika katika mashirika ya umma.

MJI WA SERIKALI: AWAMU YA PILI

Msigwa alieleza kuwa ujenzi wa mji wa serikali Awamu ya Pili umekamilika kwa asilimia 90.1, ukihusisha majengo 34 ambapo sita tayari yanatumika. Ujenzi huu unagharimu shilingi bilioni 738.9.

Aidha, miundombinu ya barabara za lami yenye urefu wa kilometa 59.1 na umeme wa chini ya ardhi wenye urefu wa kilometa 42 inaendelea. Pia, upandaji miti 233,000 umefanyika katika maeneo ya wazi na pembezoni mwa barabara.

RAIS Dk. SAMIA KUZINDUA MIRADI SIMIYU NA MWANZA

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi ya siku saba katika mikoa ya Simiyu na Mwanza kuanzia Juni 15. Katika ziara hiyo, atazindua miradi mbalimbali ya maendeleo na kufungua rasmi Daraja la Kigongo-Busisi lililokamilika kwa asilimia 100.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Samia amepata mwaliko maalum wa kufanya ziara ya kikazi Msumbiji na Visiwa vya Comoro.

VIJANA WAONYWA KUHUSU MITANDAO YA KIJAMII

Msigwa aliwaasa vijana, hususan wa vyuo vikuu, kutumia mitandao ya kijamii kwa manufaa badala ya kuichafua serikali. Alisisitiza kuwa sheria dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao ipo na vyombo vya dola vitaendelea kuchukua hatua kwa wanaovunja sheria hizo.

Kwa ujumla, hatua hizi zinaashiria dhamira thabiti ya serikali ya Awamu ya Sita katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo na kuhakikisha uwazi katika matumizi ya rasilimali za umma.

About the author

mzalendoeditor