Na.Meleka Kulwa_DODOMA
Kwa kutambua mchango mkubwa wa waendesha bodaboda na bajaji katika sekta ya usafirishaji, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Peter Mavunde, ameonesha nia ya kuwasaidia vijana hawa kwa vitendo. Tarehe 10 Juni 2025, Mavunde alihudhuria uzinduzi wa chama cha ushirika wa waendesha bodaboda na bajaji mkoani Dodoma kinachojulikana kama UMAPIDO (Ushirika wa Madereva wa Bajaji na Pikipiki Dodoma).
Katika hafla hiyo, Mavunde aliwasihi vijana wanaojihusisha na kazi ya usafirishaji ambao bado hawajajiunga na Saccos hiyo kujitokeza mara moja ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa. Alisisitiza kuwa ushirika huo utawasaidia kupata mikopo nafuu, bima, na hata mafunzo yatakayowezesha kuongeza tija katika kazi zao.
Mbunge huyo pia alitoa mchango wa Shilingi Milioni 15 kwa ajili ya kuimarisha mtaji wa Saccos hiyo, akisema kuwa lengo kuu ni kusaidia vijana kuondokana na changamoto za mikopo yenye riba kubwa ambayo mara nyingi huathiri maendeleo yao. Mavunde alisisitiza kwamba msaada huu ni sehemu ya juhudi za serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan za kuwawezesha vijana na kukuza ajira.
Naye Diwani wa Kata ya Makole, Mheshimiwa Haji Omary, aliongeza kuwa ushirika wa aina hii ni fursa kubwa kwa vijana wa kata hiyo. Alisema kuwa chama hicho kitasaidia sana vijana wa Makole na Dodoma kwa ujumla kuwa na mazingira mazuri ya kufanikisha shughuli zao za kila siku.
Hafla hii ilihudhuriwa na wadau mbalimbali, wakiwemo wawakilishi wa benki na viongozi wa serikali, ambapo kila mmoja alionyesha matumaini makubwa juu ya mafanikio ya ushirika huo katika kuboresha maisha ya vijana wa Dodoma.