MAWAZIRI wenye dhamana ya michezo walikutana na viongozi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Jijini Nairobi nchini Kenya kujadiliana kuhusu uratibu wa hati ya kusafiria ya pamoja (Pamoja VISA) wakati wa Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) 2024 zinazoandaliwa kwa pamoja na Kenya, Tanzania na Uganda zitakazofanyika Agosti mwaka huu.
Mawaziri hao, Profesa Palamagamba Kabudi wa Tanzania, Salim Mvuryawa Kenya na Peter Ogwang wa Uganda kwa pamoja na Maafisa wa CAF wamejadili mikakati ya maandalizi ya mashindano ya CHAN na umuhimu wa kuwepo hati ya kusafiria ya pamoja (Pamoja VISA).
Kikao hicho kimeona umuhimu huo kwa sababu itasaidia kurahisisha kuingia na kutoka kwa wachezaji, wataalamu na washabiki kwenye nchi waandaaji wakati wa mashindano hayo.
Pamoja na hilo, Mawaziri hao kwenye kikao chao na CAF walijadili mipango ya kibajeti kwa ajili ya kuwezesha mashindano na masuala ya misamaha ya kodi kwa vifaa vitakavyotumika kwenye CHAN ya Afrika Mashariki.
Pamoja na Mawaziri na viongozi na wataalamu kutoka CAF, kikao hicho pia kilihudhuriwa na Makatibu wakuu, marais wa mashirikisho ya Soka ya nchi hizo, Wenyekiti wa kamati za maandalizi za kitaifa (LOC’s).