Featured Kitaifa

WANAFUNZI 149,818 WACHAGULIWA KUJIUNGA KIDATO CHA TANO

Written by mzalendoeditor

WAZIRI Wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Mhe.Mohamed Mchengerwa ,akizungumza na Waandishi wa Habari leo Juni 6,2025 jijini Dodoma  kuhusu uchaguzi wa Wanafunzi wakujiunga na kidato Cha Tano na vyuo vya Elimu ya ufundi Kwa Mwaka 2025.

Na.Meleka Kulwa-DODOMA

Jumla ya Wanafunzi 149,818 sawa na asilimia 69.96 wakiwemo wasichana 76,491 na wavulana 73,327 wenye sifa wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano katika Shule 694 za sekondari za Serikali.

141,146 waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka, 2024,wenye sifa wakiwemo wasichana 72,337 na wavulana 68,809 wamepangwa katika shule za bweni na Wanafunzi 6,944 wakiwemo wasichana 3,353 na wavulana 3,591 wamepangwa katika shule za kutwa.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Juni 6,2025 na Waziri Wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Mohamed Mchengerwa  wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu uchaguzi wa Wanafunzi wakujiunga na kidato Cha Tano na vyuo vya Elimu ya ufundi Kwa Mwaka 2025.

Waziri Mchengerwa  amesema jumla  ya wanafunzi laki 214,141 wakiwemo wasichana elfu 97,517 na wavulana laki 116,624 ambao walikuwa na sifa za kuchaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo vya Elimu ya Ufundi ikijumuisha wanafunzi 1,028 wenye mahitaji maalum.

Aidha Mchengerwa ameeleza  kuwa Wanafunzi hao  wenye sifa wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano katika Shule  694 za sekondari za Serikali  ambapo Wanafunzi elfu 1,728 wakiwemo wasichana 801 na wavulana 927 wamepangwa katika shule za sekondari 8 zinazopokea wanafunzi wenye ufaulu wa juu zaidi.

Wanafunzi 2,875 wakiwemo wasichana 1,057 na wavulana 1,818 wamechaguliwa kujiunga na fani mbalimbali katika Vyuo 04 vya Elimu ya Ufundi, vyuo hivyo ni Chuo cha Ufundi cha Arusha (ATC), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) na Chuo cha Maendeleo ya Maji (WMDI)

Pia amebainisha kuwa Wanafunzi 2,214 wakiwemo wasichana 1,099 na wavulana 1,115 wamechaguliwa kujiunga na Vyuo vya Afya ngazi ya Stashahada, Wanafunzi 1,609 wakiwemo wasichana 443 na wavulana 1,166 wamechaguliwa kujiunga na Vyuo vya Ualimu kozi za Stashahada na Wanafunzi 57,625 wakiwemo wasichana 18,427 na wavulana 39,198 wamechaguliwa kujiunga na Vyuo vya Kada mbalimbali. 

“Muhula wa kwanza kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano utaanza tarehe 08 Julai, 2025. Hivyo Wanafunzi wote waliopangwa kujiunga na Kidato cha Tano kwa mwaka, 2025 wanapaswa kuanza kuripoti Shuleni kuanzia tarehe 06 Julai, 2025 na kwamba . Siku ya mwisho ya kuripoti itakuwa tarehe 21 Julai, 2025.

Hata hivyo,Waziri Mchengerwa amefafanua kuwa  kwa wanafunzi waliopangwa kwenye Vyuo vya Elimu ya Ufundi watapokea maelekezo ya namna ya kujiunga kutoka katika Vyuo walivyopangwa. 

“Uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo umefanyika kwa kuzingatia ufaulu na nafasi zilizopo; hivyo, hakutakuwa na fursa ya kufanya mabadiliko yoyote ya Shule kutokana na ukosefu wa nafasi,”Amesisitiza Waziri Mchengerwa.

Hata hivyo ametumia fursa hiyo kuwapongeza walimu, wazazi na walezi wote kwa juhudi walizozifanya katika malezi na ufundishaji hali iliyowezesha wanafunzi kufaulu vizuri.

Aidha Waziri Mchengerwa amewaomba wazazi,walezi wote waendelee na moyo  wa kusimamia na kufuatilia maendeleo ya watoto huku  akiwapongeza wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo vya Elimu ya Ufundi.

About the author

mzalendoeditor