Featured Kitaifa

WAGANGA WAKUU WA MIKOA HAKIKISHENI HOSPITALI ZA WILAYA ZINALEA VITUO VYA AFYA

Written by mzalendo

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia afya Prof. Tumaini Nagu amewaelekeza Waganga Wakuu wa Mikoa (RMO`S) Kuhakikisha Hospitali zote za Wilaya Nchini zinalea vituo vilivyopo chini yao ili kufanikisha upatikani wa huduma bora za afya kwenye vituo vyote vya ngazi ya afya Msingi.

Prof. Nagu ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara ya usimamizi shirikishi katika Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani.yenye lengo la kuangalia upatikanaji wa huduma za afya, lishe na ustawi wa jamii katika Mkoa huo.

“Waganga Wakuu wa Mikoa wote hakikisheni huduma bora zinazotolewa ikatika hospitali za wilaya, vivyo hivyo hospitali hizo zilee vituo vya afya vilivyopo chini yake navyo viweze kutoa huduma bora na vituo vya afya vitalea Zahanati za maeneo husika” amesisitiza.

Aidha, Prof. Nagu amewapongeza Watumishi wa Hospitali ya wilaya ya Mkuranga kwa uhamasishaji mkubwa kwa wananchi wa Mkuranga katika uchangia mkubwa wa damu na kufanya kuwe na hazina ya kutosha.

“Tumeona kuna damu nyingi kwenye majokofu yenu ya kuhifadhia damu na kuna utunzaji mzuri pia katika maabara zenu, na kumekuwa na muitikio mkubwa wa wananchi kuchangia damu hii imetokana na elimu ambayo mmekuwa mkitoa kwa wananchi”

Pia, ameipongeza Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga kwa kuwa na maabara bora yenye ithibati ambayo inahakikishia ubora wa majibu ya vipimo hivyo kuwezesha matibabu sahihi.

About the author

mzalendo