Featured Kitaifa

MIRADI YENYE THAMANI YA BILIONI 4.3 YATEKELEZWA KATA YA BOLISA, KONDOA MJINI

Written by mzalendoeditor


Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Mji wa Kondoa, Hassan Kiseto,akizungumza leo Juni 3, 2025, wakati wa maadhimisho ya SAMIA DAY, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo.

Diwani wa Kata ya Bolisa Hajat Ramla Abedi akizungumza leo Juni 03, 2025 wakati wa maadhimisho ya SAMIA DAY katika viwanja vya shule ya msingi Bolisa iliyopo Tarafa ya Kolo Halmashauri ya Kondoa Mji , Mkoani Dodoma

NA Okuly Julius , KONDOA

Katika kipindi cha miaka minne (2021/22 hadi 2024/25), Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuonesha dhamira ya kweli ya kuwaletea wananchi maendeleo, kwa kutekeleza miradi mikubwa 15 katika Kata ya Bolisa, Halmashauri ya Mji wa Kondoa, yenye thamani ya shilingi bilioni 4.29.

Akizungumza leo Juni 3, 2025, wakati wa maadhimisho ya SAMIA DAY, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Mji wa Kondoa, Hassan Kiseto, alisema kuwa miradi hiyo imehusisha sekta za elimu, afya, maji, barabara, umeme na maendeleo ya jamii.

“Maendeleo haya ni ushahidi wa namna serikali ilivyojipanga kuleta mabadiliko ya kweli kwenye maisha ya Watanzania wa kawaida, hasa katika maeneo ya vijijini kama Bolisa,” alisema Kiseto.

Kiseto alibainisha kuwa kata hiyo yenye wakazi 3,919 ina shule mbili za msingi zenye wanafunzi 822 na shule mbili za sekondari zenye wanafunzi 310. Katika kipindi hicho, serikali imewekeza sana katika sekta ya elimu kwa lengo la kuinua kiwango cha taaluma na mazingira ya kujifunzia.

Katika elimu ya msingi, miradi iliyotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba ya mwalimu Shule ya Msingi Itiso kwa zaidi ya shilingi milioni 4.58, na ujenzi wa chumba cha darasa pamoja na ofisi mbili za walimu kwa zaidi ya shilingi milioni 4.2. Miradi hii inatarajiwa kukamilika mwaka wa fedha 2025/26.

Kwa upande wa elimu ya sekondari, Shule ya Sekondari Bolisa imejengwa kwa zaidi ya shilingi milioni 546. Pia, Shule ya Sekondari Gubali imenufaika na ujenzi wa madarasa 12, mabweni 2, matundu ya vyoo 18 na ofisi moja, kwa jumla ya shilingi milioni 604.

“Tumeshuhudia mabadiliko makubwa ndani ya muda mfupi. Hili ni zao la maono ya Rais wetu mpendwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amedhamiria kubadilisha elimu nchini,” alisema Kiseto.

Katika miundombinu ya barabara, serikali imekamilisha barabara ya changarawe ya Gubali – Bolisa – Iboni yenye urefu wa kilomita 14.7 kwa gharama ya shilingi milioni 386. Kiseto alisema barabara hiyo tayari inatoa huduma kwa wananchi kwa ufanisi mkubwa.

“Awali ilikuwa ni changamoto kusafirisha wagonjwa au mazao, lakini sasa barabara ni imara na inapitika kipindi chote cha mwaka,” alieleza.

Mradi mwingine mkubwa ni barabara ya Iboni–Bolisa–Gubali, ambayo utekelezaji wake umefikia asilimia 98 kwa gharama ya shilingi milioni 756.

Kwa upande wa maji, kata hiyo imenufaika na usambazaji wa maji safi katika mitaa ya Bolisa na Poisi kwa gharama ya shilingi milioni 643. Mradi huo tayari unafanya kazi na umeleta unafuu mkubwa kwa wakazi wa maeneo hayo.

“Kwa mara ya kwanza, wakazi wa Bolisa wamepata huduma ya maji safi ya bomba majumbani. Wanawake sasa hawalazimiki kutumia muda mwingi kutafuta maji,” alisema Kiseto.

Sekta ya nishati pia haijaachwa nyuma. Mradi wa usambazaji wa umeme katika mitaa yote ya kata hiyo umetekelezwa kwa zaidi ya shilingi milioni 159, hatua ambayo imechochea shughuli za kiuchumi na kijamii.

Aidha, kupitia mchango wa wafadhili, zaidi ya shilingi milioni 245 zimetolewa kwa ajili ya kuwawezesha kaya maskini kujikwamua kiuchumi kupitia miradi ya kilimo, ufugaji na biashara ndogondogo.

Kwa ujumla, kati ya shilingi bilioni 4.29 zilizowekezwa katika miradi hiyo:Serikali Kuu imetoa zaidi ya shilingi bilioni 3.9,Wananchi wamechangia shilingi milioni 105, na Wahisani wamechangia zaidi ya shilingi milioni 290.

Halmashauri ya Mji wa Kondoa haijachangia moja kwa moja fedha, lakini imesimamia na kuratibu miradi yote kikamilifu.

“Mafanikio haya ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi na dira ya maendeleo ya Taifa. Wananchi wa Bolisa wana kila sababu ya kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita,” alihitimisha Kiseto.









About the author

mzalendoeditor