WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Mei 27,2025 jijini Dodoma.


WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Mei 27,2025 jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda,ameweka wazi mafanikio ya sekta ya elimu katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, huku akisisitiza kuwa mageuzi yaliyofanywa ni ya kihistoria na ya kimkakati, yakilenga kuijenga Tanzania ya ujuzi.
Prof.Mkenda ameyasema hayo leo Mei 27,2025 jijini Dodoma ,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Prof. Mkenda amesema kuwa mafanikio haya ni matokeo ya maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika elimu, Sayansi na Teknolojia.
“Rais wetu ameongeza bajeti, amezindua sera mpya, na kuhakikisha kila Mtanzania anapata elimu bora, jumuishi na yenye ujuzi,” amesema Prof. Mkenda.
Kuhusu Sera Mpya na Mitaala Inayozingatia Ujuzi alisema kuwa Mojawapo ya hatua kubwa zilizopigwa ni uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023.
“Sera hiyo imeongeza muda wa elimu ya lazima kuwa miaka 10 na kuweka muundo mpya wa elimu wa 1+6+4+2/3+3+,Aidha, mitaala mipya imeandaliwa kuanzia elimu ya awali hadi elimu ya juu, ikijumuisha mikondo miwili kwa sekondari,elimu ya jumla na ya amali,”amesema
Aidha ameeleza kuwa Mitaala 389 ya elimu ya ufundi na 563 ya elimu ya juu imehuishwa, huku somo la biashara na historia ya Tanzania likiwa la lazima.
Lugha, TEHAMA na elimu jumuishi pia zimetiliwa mkazo, huku mwongozo wa matumizi ya teknolojia na AI ukitolewa kwa mara ya kwanza nchini.
Hata hivyo Prof.Mkenda amesema kuwa Kupitia mradi wa HEET wenye thamani ya Shilingi bilioni 972, Serikali imejenga majengo ya elimu ya juu kwenye mikoa 16 ambayo haikuwa na vyuo vikuu, yakiwemo maabara, mabweni na madarasa.
Amesema kuwa Mradi huo unaongeza upatikanaji wa elimu ya juu na kupunguza uhaba wa wahadhiri kwa asilimia 20.
Ameeleza kuwa Rais Samia ameongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kutoka Sh bilioni 570 mwaka 2021/22 hadi bilioni 787 mwaka 2024/25.
Idadi ya wanufaika imeongezeka kwa asilimia 39.6, kufikia wanafunzi 248,331. Aidha, tozo mbalimbali zimeondolewa, na fedha za kujikimu zimepandishwa kutoka Sh 8,500 hadi Sh 10,000 kwa siku.
Wanafunzi wa stashahada pia wamepata mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 19.95, ongezeko la asilimia 177.6 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Kupitia Samia Scholarship, wanafunzi 1,343 wanaosomea sayansi na teknolojia wamefadhiliwa, baadhi hadi shahada za juu katika teknolojia ya nyuklia.
“Serikali imekamilisha vyuo vya VETA 29, huku ujenzi ukiendelea katika vyuo 64 vya wilaya na chuo kimoja cha mkoa, Chuo kipya cha ufundi Dodoma chenye uwezo wa wanafunzi 3,000 kimejengwa, na Zanzibar kimeanzishwa Chuo cha Teknolojia cha India (IIT) kinachofundisha AI, Robotics na Machine Learning.”amesema
Prof. Mkenda amesema kuwa Mafanikio hayo ni kielelezo cha dhamira ya kweli ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuweka msingi thabiti wa taifa lenye ujuzi, ubunifu na maendeleo ya kweli, Elimu na ujuzi sasa ni mpango mzima.