WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana,akiwasilisha leo Mei 19,2025 bungeni jijini Dodoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WIZARA ya Maliasili na Utalii itaendelea kutumia teknolojia katika kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu kwa kununua ndege nyuki (drones) 12 na mikanda maalum ya mawasiliano 50 (GPS Satellite Collars) kwa ajili ya ufuatiliaji wa mienendo ya wanyamapori hao.
Hayo yameelezwa leo bungeni Mei 19,2025 na Waziri wa Wizara hiyo Dk Pindi Chana wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Waziri Chana amesema Mikanda hiyo itafungwa kwa tembo viongozi katika maeneo yenye changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu.
Vilevile, Wizara itanunua na kusambaza mabomu baridi 40,000 katika maeneo yenye changamoto ya Tembo.
“Wizara itaendelea kufanya tafiti za kimkakati kwa ajili ya kugundua mbinu mpya za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu.”amesema Dkt.Chana