Waraka uliovuja unaodai kuwa ni mkakati wa siri wa Shirika la Marekani la Misaada ya Kimataifa (USAID) kusaidia viongozi wa upinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Tanzania mwaka 2025 umeibua mjadala mkali ambapo Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam umekanusha nyaraka hizo.
Waraka huo wenye kichwa cha habari “Mission – Tanzania 2025 Elections Action Plan” unadai kuwa USAID, chini ya mwavuli wa kukuza demokrasia na utawala bora, imepanga kutoa fedha kwa ajili ya kuimarisha nafasi ya kisiasa na kusaidia baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani, wakiwemo wa CHADEMA na ACT-Wazalendo.
Pia waraka huo unaeleza kuhusu uratibu wa shughuli za uangalizi wa uchaguzi kutoka Marekani, utoaji wa elimu kwa wapiga kura, pamoja na mipango ya kukabiliana na migogoro ya kisiasa kupitia kikundi kazi maalum cha ubalozi.
Hata hivyo, Ubalozi wa Marekani umejibu kwa ukali na kukanusha kuwa waraka huo si wa kweli.
“Tumejiridhisha kuwa nyaraka hizi si sahihi na hazionyeshi sera ya Ubalozi wa Marekani kuhusu uchaguzi,” ilisema taarifa ya ubalozi huo iliyotolewa Ijumaa.
Viongozi wa CHADEMA na ACT-Wazalendo pia hawakutoa maoni, wakidai bado wanausoma waraka huo. Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia Katibu wa Halmashauri Kuu – Itikadi, Uenezi na Mafunzo CPA Amos Makalla, alilithibitisha kupokea taarifa hizo na kusema wanazifanyia uchambuzi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi, alisema hana taarifa kuhusu waraka huo lakini aliahidi kufuatilia ili kubaini ukweli wake.
Akizungumza na HabariLEO, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ramadhan Kailima, alikanusha kuhusika kwa tume hiyo, akisema: “INEC haihusiki na namna vyama vya siasa vinavyopata fedha au vifaa vya uendeshaji – hilo linasimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.”
Hata hivyo, Kailima alithibitisha kuwa USAID ni miongoni mwa taasisi zilizopata kibali cha kushiriki katika zoezi la uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura.
“Tulifungua rasmi maombi ya vibali vya utoaji wa elimu kwa wapiga kura na uangalizi wa uchaguzi kuanzia Aprili 21 hadi Mei 20, 2025,” alieleza.
Wakati hisia zikiongezeka kuhusu waraka huo, baadhi ya wanaharakati wa kiraia wameuita kuwa wa kutungwa na wenye malengo ya kisiasa.
“Hii ni njama ya makusudi ya kudhoofisha vyama vya upinzani,” alisema mchambuzi mmoja mashuhuri aliyeomba kutotajwa jina, huku akielekeza lawama kwa CCM. Hadi sasa chama hicho hakijatoa msimamo rasmi.
Wakati huohuo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki haijatoa tamko lolote, ingawa jitihada za kupata msimamo wake zinaendelea.
Uvujaji wa waraka huu umekuja wakati hali ya kisiasa ikizidi kuwa na mvutano kuelekea uchaguzi. CHADEMA, chama kikuu cha upinzani, kimesema hakiwezi kushiriki uchaguzi mkuu ujao iwapo mchakato hautafanyiwa marekebisho ya msingi, hususan kuhusu tume ya uchaguzi, wakisisitiza kuwa uchaguzi huo unapaswa kuwa huru na wa haki.
Kwa upande wake, serikali imesisitiza kuwa mageuzi muhimu tayari yamefanyika, yakiwemo kuanzishwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).