Featured Kitaifa

BODI YA NISHATI VIJIJINI (REB) YATOA WITO KWA WANANCHI KULINDA MIUNDOMBINU YA UMEME VIJIJINI MKOANI KILIMANJARO

Written by mzalendoeditor

Wajumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) wametoa wito kwa Wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro kulinda miundombinu ya Miradi ya umeme vijijini pamoja na kuwaomba wawe walinzi ili kupunguza wizi wa vifaa na uharibifu unaofanywa na Wananchi wasio rai wema.

Wito huo umetolewa na Mhe. Balozi, Radhi Msuya kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi hiyo inayoisimamia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) tarehe 16 Mei, 2025 wakati wa majumuisho ya ziara yao katika mkoa wa Kilimanjaro katika kitongoji cha Shabaha na Mjohoroni katika Halmashauri ya wilaya ya Hai, mkoani humo.

Mhe. Balozi Radhia amesema umeme ni moja ya nyenzo muhimu ya kuinua uchumi wa Wananchi mijini na vijijini, kwa sababu hiyo, wizi wa miundombinu unarudisha nyuma juhudi za Serikali katika kuwaletea Wananchi maendeleo.

“Wito wangu kwa Viongozi wa mitaa wawahamasishe Wananchi ili wajue thamani ya hii Miradi ya Serikali iliyojengwa kwa fedha nyingi, ili tuweze kufikia adhima ya maendeleo endelevu”. Amekaririwa Mhe. Balozi, Radhia Msuya.

Naye Mhandisi, Emmanuel Yesaya, Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji Miradi ametoa woto kwa Wananchi wa vitongoji vya Shabaha na Mjohoroni kuchangamkia fursa ya kujiunga na huduma ya umeme wakati huu ambapo Wakandarasi bado wapo kwenye maeneo ya Miradi kwa ajili ya kujiletea maendeleo.

Naye Meneja wa TANESCO wilaya ya Hai; Mhandisi, Joseph Bagabuje amesema Shiriki hilo, wilayani Hai kwa kushirikiana na Viongozi wa vitongoji wameanza kuwahamasisha Wananchi wa maeneo ilipo Miradi hiyo ili kuongeza idadi ya Wananchi watakajiunganisha na huduma ya umeme.

“Tumeanzisha kitu kinaitwa “mobile clinic”. Lengo ni kuwafuata Wananchi kwenye maeneo yao na kutatua changamoto zao kwenye masuala yote ya umeme lakini pia wanaunganishwa (Connection) na huduma ya umeme ndani ya siku mbili baada ya Mteja kulipa”. Amekaririwa, Mhandisi Bagabuje.

Jumla ya Vitongoji 135 vinatarajiwa kufikiwa na Umeme katika Mradi (HEP II) unaosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa mkoa wa Kilimanajaro.

About the author

mzalendoeditor