Featured Kitaifa

WANANCHI WAPATAO 3000 WAPATIWA VIBALI VYA KUINGIA KATIKA HIFADHI YA MSITU KIGHOSI

Written by mzalendoeditor

Na Anangisye Mwateba

Serikali imetoa fursa kwa wananchi kufanya shughuli za kiuchumi katika hifadhi za misitu wa Kigosi ambazo ni ufugaji wa nyuki, uchimbaji wa madini, uvuvi, utalii wa aina mbalimbali, utafiti na mafunzo ambapo hadi sasa wafugaji nyuki wapatao 3,061 kutoka katika vijiji 105 wamepewa vibali vya kuingia ndani ya hifadhi na wameweza kutundika mizinga ya nyuki ipatayo 585,713.

Haya yamebainika leo wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni ambapo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula (Mb) akijibu swali la Mhe. Nicodemas Henry Maganga aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuwagawia sehemu ya eneo la Pori la Kigosi ili Wananchi waweze kulitumia kwa shughuli za kiuchumi.

Hifadhi ya Msitu Kigosi ilianzishwa kwa Tangazo la Serikali Na. 345 la tarehe 03/05/2024 ikiwa ni Hifadhi ya Serikali Kuu inayosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania. Hifadhi hii inapakana moja kwa moja na vijiji 54 vinavyopatikana katika Wilaya sita (6) ambazo ni Biharamulo – Kagera, Bukombe na Mbogwe – Geita, Kahama (Halmashauri ya Ushetu) – Shinyanga, Kaliua – Tabora na Kakonko katika Mkoa wa Kigoma. Eneo kubwa la hifadhi hii lipo katika Wilaya za Bukombe na Kahama.

Malengo ya kuhifadhi eneo hili ni kuwezesha masuala mawili ya msingi ambayo ni uhifadhi wa baionuai ya mimea na Wanyama ili kuwezesha upatikanaji wa huduma za kiikolojia kama maji, kupambana na kuhimili mabadiliko ya tabia nchi na kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi kwa jamii na Taifa kwa jumla.

About the author

mzalendoeditor