Featured Kitaifa

WATAALAMU WA MABONDE WATAKIWA KUJIKITA KUFANYA UTAFITI WA MAJI CHINI YA ARDHI

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewataka wataalamu wa Mabonde kujikita katika kufanya utafiti wa maji chini ya ardhi ili huduma ya maji kwa wananchi iwe endelevu.

Mhe. Aweso ameyasema hayo leo Mei 9, 2025 wakati akikabidhi vifaa vya kisasa vya utafiti wa maji chini ya ardhi vilivyonunuliwa kwa fedha za UVIKO.

“Vifaa hivi viwe chachu ya kuwaongezea uwezo wataalamu wetu na kuweka nguvu katika utafiti ili maeneo yaliyokuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji yapate maji” Waziri Aweso amesema ambapo vifaa hivyo vinagawanywa katika mabonde tisa ya maji.

Mkurugenzi wa Idara ya Rasilimali za Maji Dkt. George Lugomela amesema vifaa hivyo vitawezesha kuchunguza uwepo wa miamba inayohifadhi maji kwa ufanisi hadi kina cha urefu wa mita 1000.

Vifaa hivyo ni pamoja na kifaa cha kuchunguza mipasuko katika miamba kwa njia ya sumaku (Magnetrometer), kifaa cha kuchunguza maji (terrameter),kifaa cha kupima kina cha maji (deeper),kifaa cha kuchunguza mikondo ya maji na kifaa cha kuchukua majira (GPS).

Mkurugenzi Lugomela amemshukuru Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha kwa fedha zinazosaidia kufikisha azma ya kupata huduma ya maji kwa wananchi kwa asilimia 85 vijijini na 95 mjini ifikapo 2025.

About the author

mzalendoeditor