Featured Kimataifa

RAIS SAMIA NA RAIS CHAPO WAKUBALIANA KUENDELEZA USHIRIKIANO WA KIUCHUMI  BAINI YA TANZANIA NA MSUMBIJI 

Written by mzalendoeditor

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimpokea mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Daniel Francisco Chapo mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 08 Mei, 2025

…..

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri  ya Msumbiji, Mhe. Daniel Francisco Chapo wamekubaliana kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi  baina ya Tanzania na Msumbiji hususan katika eneo la biashara na uwekezaji kwa kuanzisha Tume  ya Pamoja ya Uchumi (JEC) ili kutatua changamoto za kiuchumi. 

Makubaliano hayo yamefikiwa leo katika majadiliano ya mazungumzo rasmi baina ya Marais hao wawili yaliyofanyika, Ikulu jijini Dar es Salaam. 

Aidha, Rais Dkt. Samia na Rais Chapo wamekubaliana kuendelea kuboresha mazingira ya biashara  na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili, ikiwemo kuwawezesha wajasiriamali na wafanyabiashara  wadogo na wa kati kufanya biashara kwa urahisi (Simplified Trade Regimes – STRs).  

Kwa kutambua kuwa asilimia kubwa ya uchumi wa Msumbiji na Tanzania unategemea kilimo, nchi  hizo mbili zimekubaliana kuimarisha ushirikiano kwenye sekta hiyo, ikiwemo kubadilishana  uzoefu na kufanya tafiti za pamoja, hususan kwenye zao la korosho ili kufaidika na bei ya soko la  dunia na kuanzisha Umoja wa nchi zinazozalisha korosho na kuuza korosho zilizochakatwa. 

Mbali na kuimarisha ushirikiano kwenye sekta ya gesi ambayo Msumbiji amepiga hatua kubwa  katika sekta hiyo, Rais Dkt. Samia na Rais Chapo wamekubaliana kushirikiana katika fursa  zinazotokana na uchumi wa buluu, zikiwemo uvuvi, utalii, madini na usafirishaji, kufanya kazi kwa  karibu na kubadilishana uzoefu kwenye masuala ya uvuvi wa bahari kuu.  

Vile vile, wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya ulinzi na usalama hasa katika  kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka. 

Kwa upande mwingime, Rais Dkt. Samia amempongeza Rais Chapo kwa jitihada alizozifanya ndani  ya muda mfupi, hususan katika kujenga umoja wa kitaifa na kurejesha amani na utulivu nchini  Msumbiji. 

1/2

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA 

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS, IKULU 

Mara baada ya mazungumzo hayo, Rais Dkt. Samia na Mgeni wake Rais Chapo walishuhudia utiaji  wa saini wa Mikataba miwili ya Uanzishwaji wa Kituo cha Huduma cha Pamoja Mpakani (OSBP)  kwenye mpaka wa Mtambaswala na Negomano, ili kurahisisha ufanyaji biashara pamoja na  Mkataba wa Kubadilishana Wafungwa.  

Vilevile walishuhudia utiaji saini wa Hati nne za Makubaliano (MOU) ya Ushirikiano katika Sekta  ya Elimu, Sekta ya Utamaduni, Udhibiti wa Madawa, pamoja na ushirikiano katika Redio ya Taifa  ya Msumbiji na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) 

Wakizungumza na vyombo vya habari, Rais Chapo amesema ipo haja ya kuzidisha mahusiano  katika uchumi na biashara kwa kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, hivyo ameeleza umuhimu wa kuendelea na ujenzi wa barabara zinazounganisha Msumbiji na Tanzania. 

Rais Chapo pia amesema ni muhimu kufanya mapitio ya Mkataba wa Ushirikiano wa Usafiri Anga  kwa Mashirika ya ndege ya Msumbiji na Tanzania ili kutoa huduma kwenye miji mikubwa pamoja  na kuimarisha usafiri wa baharini. 

Rais Chapo alieleza umuhimu wa nchi hizo mbili kuimarisha vikao vya ujirani mwema katika mikoa  ya mpakani ya Ruvuma na Mtwara kwa upande wa Tanzania na Nyasa na Cabo Delgado kwa  upande wa Msumbiji. 

Katika hatua nyingine, Msumbiji imejitoa rasmi kuwa mbia wa Kituo cha Uhusiano wa  Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (CFR) kwa kuwa wameanzisha Chuo chao wenyewe na  hivyo nchi hizo mbili zitaendelea kubadilishana uzoefu kupitia vyuo hivyo. 

Wakati huo huo, Rais Dkt. Samia ameridhia mualiko wa Rais Chapo wa kuhudhuria sherehe za  Maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Msumbiji yatakayofanyika tarehe 25 Juni, 2025. 

Rais Chapo anatarajia kuhitimisha ziara yake nchini hapo kesho ambapo ataagwa rasmi na Rais Dkt.  Samia katika Ikulu ya jijini Dar es Salaam.  

About the author

mzalendoeditor