Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mhe.Aida Kenani,amempongeza Waziri wa Maji Mhe.Jumaa Aweso, Naibu wake na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kwa uadilifu na utendaji wao wa kazi, lakini akasisitiza kuwa mafanikio yoyote hayawezi kufikiwa iwapo wizara haitapatiwa fedha za kutosha katika kutekeleza miradi hiyo.
Mhe.Kenani ametoa pongezi hizo leo Mei 8,2025 jijini Dodoma wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Amesema kuwa pamoja na Serikali kupeleka miradi ya maji katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Nkasi, bado baadhi ya maeneo yanaendelea kukabiliwa na changamoto ya muda mrefu ya uhaba wa maji.
“Ili Miradi ya maji iweze kukamilika kwa wakati Waziri Aweso anahitaji pesa itoke kwa wakati “
Aidha Kenani ameitaka Serikali kuangalia pia uwezekano wa kutekeleza miradi ya muda mfupi wakati miradi mikubwa ya muda mrefu kama wa Ziwa Tanganyika ikiendelea kufanyiwa utekelezaji.
Hata hivyo ameishauri Serikali kuonesha dhamira ya dhati katika kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika mkoa wa Rukwa, hususan katika mamlaka ya mji mdogo wa Namanyere, ambako amesema kiwango cha upatikanaji wa maji bado kipo chini ya asilimia 50.
“Mheshimiwa Waziri, jambo hili nimelizungumza kwa miaka mitano. Suluhisho la msingi ni kutoa maji kutoka Ziwa Tanganyika na kuyasambaza katika mkoa wa Rukwa. Sasa tunataka kujua, hili jambo limefikia wapi?” amesema Kenani.