Chuo cha Uhasibu Arusha( IAA) kimekabidhi eneo kwa mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo la Utawala na jengo la Maktaba na Maabara ya TEHAMA katika Kampasi ya Babati.
Makabidhiano hayo yamefanyika Mei 06, 2025 Babati mjini, mahali ilipo Kampasi ya Babati mkoani Manyara.
Mkuu wa Chuo IAA Prof Eliamani Sedoyeka ameishukuru serikali kwa kuunga mkono jitihada za chuo, ambapo amesema pamoja na chuo kujenga majengo mbalimbali kwa kutumia mapato ya ndani; serikali kupitia mradi wa HEET imetoa jumla ya shilingi bilioni 48 kwa IAA, ambapo shilingi bilioni 13.7 zitatumika Babati kujenga majengo hayo.
“Uwekezaji uliofanyika katika Kampasi ya Babati unaifanya kuwa miongoni mwa miradi mikubwa mkoani Manyara na utakapoongezewa hizi bilioni 13.7 na utakuwa ni ndio mradi mkubwa kwa mkoa wa Manyara tangu uhuru, tuna mshukuru sana Mhe. Rais Dkt. SAMIA Suluhu Hassan kwa jitihada hizi za kuhakikisha kuwa wana Manyara hawaachwi nyuma katika elimu ya Juu,” alisema Prof. Sedoyeka.
Aidha, Prof. Sedoyeka amesema mradi huo ujenzi unaratajiwa kutekelezwa kwa muda wa miezi 12 chini ya mkandarasi Ami & Vai Investment Ltd na mshauri elekezi Y&P Architect (T) Ltd, ambapo amesisitiza juu ya ubora katika utekelezaji wa mradi huo ili kuendana na matarajio na ndoto za wana Manyara.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Babati, Bw. Halfan Matipula akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga amesema Serikali mkoani Manyara inajivunia uwepo wa IAA; akisisitiza kuwa mradi huo una manufaa makubwa katika uchumi wa wananchi, mkoa na taifa kwa ujumla.
Bw. Matipula amemtaka Mkandarasi kukamailisha mradi kwa wakati na viwango vinavyotakiwa, ili wananchi wapate huduma kwa wakati.
Wakati huo huo Matipula ametoa wito kwa wananchi na Viongozi mkoani Manyara kulinda na kutunza vifaa na miundombinu ya chuo.
Mradi wa ujenzi wa jengo la utawala lenye ghorofa nne na jengo la Maktaba na Maabara ya TEHAMA katika Kampasi ya Babati unatekelezwa na Mkandarasi Ami&Vai Investment Ltd chini ya Mshauri elekezi Y&P Architect (T) kwa muda wa miezi 12.