Na MwandishiWetu, Dodoma
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora nchini (THBUB) limelaani vikali kuwepo kwa matukio ya kupigwa kwa Patdri Dk.Charles Kitima ambaye ni Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na kutekwa kwa Faluka Saidi Nyagali (Mdude) wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwamba Tume hiyo imejiridhisha kuwa kuwepo kwa matukio hayo yanaashiria uvunjifu wa Haki za Binadamu pamoja na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu ameyasema hayo leo Mei 5,2025 Jijini Dodoma wakati akitoa Tamko kwa Waandishi wa Habari kuhusu kuwepo kwa matukio yanayohusiana na uvunjifu wa Haki za binadamu yaliyojitokeza hivi karibuni.
“Katika kipindi cha takriban mwezi mmoja na nusu, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imekuwa ikifuatilia kwa karibu matukio mbali mbali ambayo yamekuwa yakijitokeza nchini.
THBUB baada ya kufanya tathmini kuhusu matukio hayo kwa mujibu wa Katiba na Sheria ya THBUB, imejiridhisha kuwa matukio hayo yanaashiria uvunjifu wa haki za binadamu, ukiukwaji wa misingi ya utawala bora na uvunjifu wa amani na utulivu nchini,”amesema.
Aidha, amesema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, kumekuwa na matukio mbali mbali yakiwemo matumizi ya lugha chafu zisizozingatia utu na heshima ya mtu na zinazoleta hamasa na kuchochea uvunjifu wa amani na utulivu, matukio yanayoashiria matumizi ya nguvu kupita kiasi wakati wa kushughulikia mikusanyiko ya kisiasa, kushambuliwa na kujeruhiwa kwa baadhi ya wananchi.
Sanjari na hayo, Jaji Mwaimu amesema kutokana na matukio yaliyotokea hivi karibuni nchini THBUB imelitaka Jeshi la Polisi liendelee kuwasaka na kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika na kujeruhiwa kwa Dkt. Charles Kitima, waliomteka Faluka Saidi Nyagali (Mdude) na waliohusika katika matukio mengine ya uvunjwaji wa haki za binadamu.
Pia, ameongeza kuwa tume hiyo inaona kuwa matendo yaliyojitokeza hayatoi taswira nzuri katika ustawi wa haki za binadamu, utawala bora na amani na utulivu nchini ambayo ni muhimu sana katika kipindi hichi kuelekea uchaguzi Mkuu.
“THBUB inalaani matukio hayo ambayo yamevunja haki za binadamu na kukiuka misingi ya utawala bora na yanayoashiria uvunjifu wa amani na utulivu,”amesema.
Ameongeza kuwa THBUB inatambua kuwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi, sheria za nchi na mikataba mbalimbali ya kimataifa ya haki za binadamu ambayo Tanzania imeridhia, wananchi wote wanayo haki ya kufurahia na kupata haki zao za binadamu.
“Kwa mujibu wa Katiba ya Nchi, kila mwananchi anayo haki ya kuishi, kuwa huru, kutoa maoni na kushiriki katika shughuli za umma moja kwa moja au kupitia wawakilishi kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa katika Katiba na sheria za nchi,”ameongeza.