Featured Kitaifa

NAIBU WAZIRI MWANAIDI ATAKA WATUMISHI KUFANYA KAZI KWA BIDII NA WELEDI

Written by mzalendoeditor

NAIBU  Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Khamis,akizungumza  leo Mei 3,2025 jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo.

Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu,akizungumza  wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo.

 

Sehemu ya washiriki wakisikiliza hotuba ya Naibu  Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Khamis (hayupo pichani) wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo kilichofanyika leo Mei 3,2025 jijini Dodoma.

Mkurugenzi Idara ya Utawala na Rasimali Watu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum,Bw.Merckioni Ndofi,akizungumza wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo kilichofanyika leo Mei 3,2025 jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju,akitoa neno la shukrani kwa Mgeni rasmi Naibu  Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Khamis (hayupo pichani) mara baada ya kufungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo kilichofanyika leo Mei 3,2025 jijini Dodoma.

Na.Alex Sonna-DODOMA

NAIBU  Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Khamis,amewataka watumishi wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa bidii hasa katika kutimiza wajibu wao katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mhe. Mwanaidi ameyasema hayo leo Mei 3,2025 jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo,

Amesema kuwa ili waweze kutekeleza majukumu yao ya Wizara ni kufanya kazi kwa ushirikiano,weledi ili waendelea kuleta maendeleo kwa jamii

“Nitumie fursa hii kuwakumbusha watumishi kuwa hakuna haki bila wajibu, kwa msingi huo nimtake kila mmoja wetu kutimiza wajibu wake kwa kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma” amesema Mhe. Mwanaidi.

 Aidha,ameitaka Menejimenti ya Wizara ikiongozwa na Mwenyekiti ambaye ni Katibu Mkuu kuendelee kutoa motisha kwa watumishi wanaowajibika, wabunifu na wanaoyaishi maadili mema katika Utumishi wa Umma.

Hata hivyo amesema kuwa ili waweze kufanikiwa katika utekelezaji wa vipaumbele vya wizara kila mjumbe anayo haki na wajibu wa kutoa mawazo na ushauri kwenye utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2024/25 na mipango mipya inayohusu Bajeti ya mwaka 2025/26.

“Watumishi tujihadhari na tabia hatarishi zinazopelekea kupata maambukizi ya UKIMWI. Aidha, ninamsihi Katibu Mkuu aendelee kutoa huduma kwa waathirika wa VVU kama inavyopaswa na kwa mujibu wa bajeti.”amesisitiza 

Pia ameiagiza Menejimenti kuendelea kuboresha mazingira ya kazi ili watumishi wote waweze kufanya kazi kwa tija na ufanisi.

Katika hatua nyingine ametoa shukurani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu kwa nyongeza ya mshahara kwa watumishi wa umma ikiwa ni kuongeza chachu katika utekelezaji wa majukumu yao na maendeleo kwa Taifa.

‘Maono ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuona watumishi wa umma wanakuwa katika mazingira mazuri ya utendaji kazi wao ili kuleta maendeleo katika Taifa.”amesema 

Awali Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu ,amesema kuwa baraza hilo ni  muhimu katika kutekeleza  Dira, Dhima ya Wizara zinafikiwa na majukumu yanatekelezwa ipasavyo.

“Baraza hili ni chombo muhimu kufikia mafanikio ya Wizara, tulitumie kutathimini jinsi tulivyotekeleza majukumu yetu katika mwaka wa fedha 2024/ 2025 na kujipanga vyema kwa mwaka wa fedha 2025/2026” amesema Dkt. Jingu.

Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum limefanyika kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali ya utendaji kazi na utekelezaji wa Bajeti ya Wizara kwa Mwaka wa fedha 2024/2025 na mipango ya Bajeti ya Wizara kwa Mwaka 2025/2026.

About the author

mzalendoeditor