π *Matumizi ya kuni yawa historia*
Jeshi la Magereza Tanzania Bara limepongezwa kwa kufanikiwa kuanza kutumia mifumo ya nishati safi ya kupikia katika magereza zake zote nchini.
Pongezi hizo zimetolewa leo Aprili 30, 2025 Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali (mstaafu), Jacob Kingu wakati wa ziara yake pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy iliyolenga kukagua mifumo ya nishati safi ya kupikia katika Gereza la Isanga.
βWakala wa Nishati Vijijini (REA) imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza maono ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Mkakati wa Taifa wa Matumizi wa Nishati Safi wa Kupikia ambapo tumetoa fedha kwa ajili ya kufadhili ujenzi wa mifumo ya nishati safi ya kupikia katika Magereza pamoja na Kambi za JKT.
Leo tumetemebelea kukagua maendeleo ya mradi huo na tumeridhika kwa mabadiliko makubwa tuliyoyaona katika gereza hili. Na tumeapewa taarifa kuwa magereza yote 129 yameondokana na matumizi ya kuni na nishati zisizo rafiki kwa mazingira na sasa wameanza kutumia nishati safi ya kupikia. Kwa kweli haya ni mabadiliko makubwa sana,β amesema Mwenyekiti Kingu.
Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Jeremiah Katungu amesema kuwa gereza hilo linatumia mifumo ya gesi pamoja na mkaa rafiki kupikia hali iliyowapelekea kupunguza gharama pamoja na kutumia muda mdogo kuandaa chakula.
Naye, Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala wa REA, Mhandisi Advera Mwijage amesema kuwa licha ya kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa mifumo ya nishati safi ya kupikia katika magereza, REA pia itatoa fedha kwa ajili ya kuwezesha watumishi katika Magereza wanapata nishati safi za kupikia.
βSisi kama Wakala wa Nishati Vijijini tungependa kumshukuru sana Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha miradi hii kutekelezwa katika Magereza zetu hapa nchini na hivyo kupunguza matumizi ya kuni hali itakayopelekea kutunza mazingira yetu,β amesema Mhandisi Mwijage.
Mhandisi Mwijage pia ameendelea kutoa wito kwa Watanzania pamoja na Taasisi mbalimbali kuendelea kutumia nishati safi za kupikia ili kulinda mazingira yetu pamoja na kuokoa vifo vitokanavyo na matumizi ya nishati zisizo safi na salama za kupikia.