Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi ametembelea nyumbani kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kijijini Mwitongo na kukabidhiwa fimbo maalum na familia hiyo ya mwasisi wa Tanzania na CCM.
Balozi Nchimbi ambaye yuko ziara ya kikazi ya siku tano katika Mkoa wa Mara, mbali ya kukabidhiwa zawadi hiyo, yeye pamoja na msafara wake, pia alipata fursa ya kuweka shada la maua na kufanya misa fupi kwenye kaburi alipozikwa Mwalimu Nyerere.
Kiongozi wa Kabila la Wazanaki, Chifu Joseph Wanzagi, alimwambia Balozi Nchimbi kuwa hicho ni kifaa cha kazi atakachotumia katika dhamana alizoaminiwa kutumikia Watanzania. Alisisitiza kuwa huwa wanafanya hivyo kwa kiongozi mwenye sifa zinazofaa.
“Tunakukabidhi fimbo hii. Huwa tunakabidhi kwa kiongozi tunayemkubali. Kwa kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi utaitumia kuchapa na kuwarekebisha wale wote ambao wanataka kutatiza shughuli za uchaguzi kinyume na utaratibu wa Kikatiba,” alisema Chifu Wanzagi.
Balozi Nchimbi ambaye aliambatana na mwenza wake, Mama Jane Nchimbi, pamoja na viongozi wa Chama na Serikali Mkoa wa Mara na Wilaya ya Butiama, pia alipata fursa ya kufanya mazungumzo na Familia ya Mwalimu Nyerere, nyumbani hapo.