Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri Mkuu na Makamu wa kwanza wa Rais mstaafu Mzee John Malecela amesherehekea kumbukizi ya miaka 91 ya kuzaliwa kwake ambapo alizaliwa Aprili 20,1934 katika kijiji cha Mvumi mkoani Dodoma.
Sherehe hiyo imefanyika Aprili 20,2025 nyumbani kwake ambapo imewajumuisha wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki ambapo ametumia wasaha huo kuungana na viongozi wa dini nchini kuomba uchaguzi mkuu wa mwaka huu kuwa wa neema na amani.
“Mimi huwa sifichi kwamba ni CCM, kwahiyo naitakia kila lakheri ishinde nan chi yetu iendee kuwa ya Amani, utulivu na mshikamano,”amesema.
Aidha ametumia wasaha huo kuipongeza Serikali ya wamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utendaji wake wa kuleta maendeleo katika sehemu mbalimbali nchi hususani Dodoma ambapo amesema ni mkoa ambao upendelewa kuliko mikoa yote nchini kwani kipindi cha nyuma haukuwa na muonekano kama uluionao kwasasa.
Naye mtoto wa mzee huyo ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi mkoa wa Dodoma Samweli Malecela amesema kuwa ili kufikia umri kama huo lazima upate Baraka za Mwenyezi Mungu pamoja na kuzingatia afya yako.
“Wengi wetu tumekuwa waoga wa kuangalia afya zetu tukidhani kuwa tukienda hospitali tunaondoka na gunia la dawa sio kweli, watu wawe na utaratibu wa kuangalia afya zao na nadhani hii ndiyo siri kubwa ya baba yetu kufikisha umri huu, mara nyingi amekuwa akizingatia kanuni za afya na kula kwa wakati,”amesema.