Featured Kitaifa

NELSON  MANDELA  KUTUMIA BUNIFU KUKUZA UCHUMI KUPITIA KILIMO

Written by mzalendoeditor

Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Prof. Maulilio Kipanyula ( wa pili kulia) akizungumza na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli ( wa pili kushoto) alipomtembelea ofisini kwake Aprili 14, 2025 Jijini Dodoma.

 Na. Alex Sonna-DODOMA

Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) na Wizara ya Kilimo  wamesaini  makubaliano ya mashirikiano katika tafiti na ubunifu ili kuimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali katika sekta kilimo.

Akizungumza  jijini Dodoma mara baada ya kusaini makubaliano hayo, Makamu Mkuu wa taasisi hiyo, Prof.Maulilio Kipanyula amesema kuwa, makubaliano hayo  ni mwendelezo wa hatua za kimkakati za kuimarisha mahusiano kati ya Wizara ya Kilimo na taasisi za Elimu ya Juu na Utafiti ikiwemo Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela. 

“Hatua hii inaipa fursa taasisi yetu kuwa sehemu ya mageuzi makubwa na ya kihistoria yanayofanywa na Wizara ya kilimo katika sekta ya kilimo nchini ” amesema Prof. Maulilio Kipanyula.

Aidha ameongeza kuwa  mifumo hiyo kuwa ni pamoja na ile itakayorahisisha ukusanyaji, utunzaji na uchakataji wa takwimu mbalimbali katika sekta ya kilimo  katika kuzalisha teknolojia za kibiolojia za kupambana na magonjwa na wadudu waharibifu kwenye mazao ya kilimo cha biashara na chakula kwa uboreshaji wa mbegu, afya ya udongo, teknolojia za umwagiliaji na teknolojia za kisasa za uvunaji na uhifadhi wa mazao ya kilimo.

Anazidi kufafanua kuwa makubalianao hayo yatahusisha kufanya tafiti,  na bunifu za kisayansi katika sekta ya kilimo hususan katika maeneo ya teknolojia za kidijitali zinazo chipukia na matumizi yake , maabara za kisasa na wanasayansi wabobezi wa taasisi,  wataiongezea nguvu wizara ya kilimo katika eneo la utambuzi wa vihatarishi “risks assessment” katika mazao na bidhaa za kilimo zinazo kwenda nje ya nchi, ambapo hatua hiyo itaongeza mchango wa wizara  katika kuzalisha fedha za kigeni nchini.

 

Vilevile Taasisi ya Nelson Mandela itashirikiana na Wizara ya Kilimo katika kujenga uwezo wa watumishi na wadau wengine wa sekta ya kilimo kwa kutoa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi kupitia warsha, semina, mafunzo, na ushauri wa kitaalamu kwa wataalamu kutoka pande zote mbili pia kuhakikisha tunaongeza maarifa na ujuzi unaohitajika katika mzingira ya sasa ya kilimo yanayobadilika kwa kasi.

 

Prof. Kipanyula ameupongeza uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan hususani katika sekta ya ya Kilimo kwa mageuzi makubwa yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika na hivyo kupelekea jamii na hasa vijana kujenga imani kuwa kilimo ni shughuli ya biashara kama zilivyo biashara nyingine.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw Gerald Mweli, ameeleza kuwa ushirikiano huo hauna kikomo  na utawezesha wataalam mbalimbali wa Wizara ya Kilimo  kupata maarifa kutoka Taasisi ya NM-AIST  katika utafiti wa kilimo ili kuongeza tija kwa wakulima. 

Ameongeza kuwa Taasisi ya Nelson Mandela itasaidia katika sekta ya kilimo katika upatikanaji wa teknolojia bora za kisasa katika kupambana na visufumbufu vya  magonjwa yanayoadhiri mazao ya kilimo ambapo itaongeza tija katika uzalishaji wa mazao kwa wakulima.

Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Prof. Maulilio Kipanyula ( kulia) akibadalishana hati ya makubaliano ya ushirikiano na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli ( kushoto) mara ya hafla ya kusaini makubaliano hayo Aprili 14, 2025 Jijini Dodoma.

Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Prof. Maulilio Kipanyula ( kulia) na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli ( kushoto) wakionyesha hati ya makubaliano ya ushirikiano mara baada kusaini Aprili 14, 2025 Jijini Dodoma.

Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Prof. Maulilio Kipanyula ( wa pili kulia) akizungumza na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli ( wa pili kushoto) alipomtembelea ofisini kwake Aprili 14, 2025 Jijini Dodoma.

Wajumbe kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela na Wizara ya Kilimo wakifuatilia mawasilisho wakati wa hafla ya kusaini makubaliano ya mashirikiano Aprili 14,2025 jijini Dodoma.

 

Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Prof. Maulilio Kipanyula na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli ( katikati) wakiwa katika picha na washiriki wa hafla ya makubaliano ya ushirikiano iliyofanyika Aprili 14, 2025 Jijini Dodoma.

About the author

mzalendoeditor