WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Palamagamba Kabudi, akizungumza na Waandishi wa Habari leo Aprili 14,2025 jijini Dodoma kuhusu Mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
…….
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Palamagamba Kabudi amesema katika kuboresha sekta ya michezo nchini, Serikali imetoa shilingi bilioni 161.9 ili kukarabati na kujenga miundombinu ya michezo nchini, ikiwa pia ni sehemu ya maandalizi ya michuano ya AFCON 2027.
Prof. Palamagamba Kabudi,ameyasema hayo leo Aprili 14,2025 jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Waziri Kabudi ameeleza kuwa miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa viwanja vya mpira wa miguu Arusha na Dodoma vyenye uwezo wa kutumiwa na watazamaji elfu 32 kila kimoja kwa mara moja, ukarabati wa Uwanja wa Uhuru na Uwanja wa Benjamin Mkapa mkoani Dar es Salaam, ujenzi wa vituo vya mazoezi na kupumzika wananchi kwa Dar es Salaam na Zanzibar, ujenzi viwanja, hosteli na akademia ya michezo katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kilichopo mkoani Mwanza.
“Sekta ya michezo nchini inakuwa kwa kasi ambapo Tanzania ni kati ya nchi tatu za Afrika zilizofuzu katika mashindano saba tofauti yanayoendeshwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF).”amesema Prof.Kabudi
Amesema kuwa ili kuhakikisha shughuli za Michezo zinafanyika kwa ufanisi Serikali ya Awamu ya Sita , katika kipindi chake cha miaka Minne imeanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Michezo ambapo jumla ya shilingi bilioni 10.657 zimetolewa.
“Mafanikio mengine yaliyopatikana kupitia fedha hizo ni kujenga na kukarabati miundombinu ya michezo, kuwezesha mafunzo kwa wataalamu mbalimbali wa michezo na kuwezesha Vyama na Mashirikisho ya michezo nchini,”amesema Prof.Kabudi
Hata hivyo ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imefanikiwa kuhuisha na kuendeleza wazo la muda mrefu la ujenzi wa Sports and Arts Arena mradi huo wa kisasa, unaotarajiwa kugharimu takribani Shilingi bilioni 300 ambapo unatarajiwa kufadhiliwa kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka nchini Korea.
“Na utakapokamilika utakuwa ni moja ya vituo vikubwa vya michezo na sanaa katika Ukanda wa Afrika Mashariki, ukiwa kichocheo cha ajira, burudani, utalii na maendeleo ya vipaji vya vijana,”ameongeza.
Kuhusu Mechi ya Watani Simba na Yanga,Serikali imesema kuwa imepanga kuzungumza na wadhamini wa dabi hiyo ya kariakoo na kuwataka Watanzania na mashabiki wa dabi hiyo kuwa na subira wakati mazungumzo hayo yakiendelea.
Katika hatua nyingine Prof. Kabudi amesema kupitia R4 za Rais Samia zimesababisha kuongezeka kwa uhuru wa vyombo vya habari na kuiwezesha Tanzania kupanda kwenye viwango vya uhuru wa vyombo vya habari duniani kutoka nafasi ya 143 mwaka 2023 hadi nafasi ya 97 mwaka 2024 na imani yao itaendelea kupanda zaidi.
Prof. Kabudi amesema kuwa,Wizara hiyo imefanikiwa kuleta utulivu ndani ya sekta ya habari, ambapo Vyombo vya Habari vilivyokuwa vimefungiwa kwa makosa mbalimbali vilifunguliwa.
“Hii inaonesha jitihada za dhati za Rais Samia za kuimarisha sekta ya habari nchini, mpaka kufikia mwezi Machi mwaka huu, Tanznia ilikuwa na vyombo vya habari 1042 vilivyosajiliwa ambapo kati ya hivyo, Magazeti ni 372, Vituo vya Redio 247, Vyombo vya Habari Mtandao 355 na Vituo vya Televisheni 68,”amesema.
Prof. Kabudi ameongeza kuwa katika kuonesha utawala wa mfano kwa vitendo, ikiwemo kusimamia kwa mafanikio makubwa utekelezaji wa sheria na miongozo inayolenga kuboresha tasnia ya habari nchini, Serikali ya awamu ya sita, katika kipindi cha miaka minne, imefanikisha kuanzishwa kwa Bodi ya Ithibati ya waandishi wa habari kama inavyoelekezwa na Sheria ya Huduma za Habari Sura ya 229.
“Bodi hii, ambayo ni ya kwanza kuanzishwa tangu kupitishwa kwa sheria hiyo, ilizinduliwa rasmi tarehe 3 Machi, 2025, hili ni fanikio kubwa na la kihistoria katika kulinda na kukuza uhuru, ubora na uwajibikaji katika sekta ya habari nchini Tanzania,”ameongeza.