Featured Kitaifa

RAIS SAMIA KUZINDUA MAJENGO YA MAHAKAMA JIJINI DODOMA

Written by mzalendoeditor
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Aprili 3,2025 kuelekea katika uzinduzi wa majengo ya Mahakama,hafla inayotarajiwa kufanyika Aprili 5,2025 jijini Dodoma.
  Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Aprili 3,2025 kuelekea katika uzinduzi wa majengo ya Mahakama,hafla inayotarajiwa kufanyika Aprili 5,2025 jijini Dodoma.
MUONEKANO wa Jengo Jipya la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania lililopo jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania siku ya Jumamosi Aprili 5,2025 jijini Dodoma.
Hayo yameelezwa leo Aprili 3,2025 jijini Dodoma na  Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel,wakati akielezea mafanikio yaliyofanyika katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita.
Prof.Gabriel amesema kuwa jengo hilo litakuwa kubwa zaidi barani Afrika miongoni mwa majengo ya makao makuu ya mahakama na kushika nafasi ya sita kwa ukubwa duniani.
“Jengo hili limejengwa kwa asilimia 100 kwa fedha za ndani kupitia kodi za wananchi, bila msaada wa Benki ya Dunia. Jumla ya Shilingi bilioni 129.7 zimetumika kutekeleza mradi huu,” amesema  Prof. Gabriel.
Aidha amefafanua kuwa jengo hilo lina sehemu tatu kuu,Mahakama ya Upeo (Supreme Court), Mahakama ya Rufani, na Mahakama Kuu. Matawi hayo yanatengeneza jengo la kati litakalotumika kama ofisi za utawala, ambalo limejengwa kudumu kwa zaidi ya miaka 100.
Kwa mujibu wa Prof. Gabriel, jengo la makao makuu ya mahakama duniani lililo na ukubwa mkubwa zaidi liko barani Asia, likiwa na mita za mraba 147,000. Jengo lililokuwa likishika nafasi ya sita liko Ulaya lenye mita za mraba 53,000, lakini nafasi hiyo sasa inachukuliwa na Jengo la Mahakama ya Tanzania lenye mita za mraba 63,244.
Mbali na ukubwa wake, jengo hilo litakuwa na mifumo ya kisasa ya TEHAMA, akili bandia, maroboti ya kuwaelekeza watu kwenye ofisi mbalimbali, pamoja na sehemu ya kutua helikopta.
Hata hivyo amesema kuwa katika uzinduzi huo, miradi mingine miwili pia itazinduliwa, ikiwemo Jengo la Makao Makuu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama lenye ghorofa sita, ambalo limegharimu Shilingi bilioni 14.3, na makazi ya majaji yenye thamani ya Shilingi bilioni 42.3.
“Ni historia kwa nchi yetu kwa serikali kujenga nyumba za mahakama kwa idadi hii,” amesema  Prof. Gabriel.
Ameeleza kuwa  maandalizi ya hafla hiyo yamekamilika, ambapo wageni wapatao 2,500, wakiwemo kutoka mahakama, serikali, bunge, mashirika mbalimbali na viongozi wa dini, wanatarajiwa kuhudhuria.

About the author

mzalendoeditor