Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwasha Mwenge wa Uhuru kuashiria uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa Mwaka 2025 katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha mkoani Pwani leo tarehe 02 Aprili 2025.
….
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zitaendelea kusimamia kwa dhati na kwa haki misingi ya demokrasia na kuhakikisha wananchi wanatumia haki yao ya kikatiba ya kushiriki uchaguzi kwa uhuru, kwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kuchagua viongozi wenye sifa wanaowataka katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizindua Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa Mwaka 2025 katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha mkoani Pwani. Ametoa wito kwa wananchi wote hususan vijana kuwa waangalifu na watu wasioitakia mema nchi kwa kuepuka kutumiwa vibaya kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani.
Makamu wa Rais amesema Wadau wote wa uchaguzi, hususan vyama vya siasa wanahimizwa na kukumbushwa kuwa wana wajibu mkubwa katika kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika katika hali ya amani na utulivu, kwa kuendesha kampeni zenye staha na kuzingatia Sheria na miongozo mbalimbali ya uchaguzi. Ameongeza kwamba Uchaguzi Mkuu unafanyika kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ibara ya 42(2) na 65, Sheria ya Uchaguzi Na. 1 ya Mwaka 2024 pamoja na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Na. 4 ya mwaka 2018.
Halikadhali Makamu wa Rais ameagiza Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa, ili waweze kutekeleza jukumu la kizalendo walilokabidhiwa la kuhakikisha kuwa wanawafikia wananchi na kuwapa taarifa sahihi kuhusu sera, mipango, miradi na mikakati ya Serikali katika kuwaletea Maendeleo.
Vilevile Makamu wa Rais amesema Mbio za Mwenge pamoja na mambo mengine zitaangazia masuala ya lishe bora, mapambano dhidi ya rushwa, mapambano dhini ya VVU na UKIMWI, mapambano dhidi ya dawa za kulevya pamoja na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria.
Makamu wa Rais amesema wazo la kukimbiza mwenge wa uhuru nchi nzima na kila mwaka lilitolewa na Vijana wa TANU katika kikao chao kilichofanyika tarehe 26 Juni, 1964. Lengo kuu likiwa ni kutekeleza kwa vitendo azma ya Baba wa Taifa ya kuhamasisha umoja, upendo, amani na ujenzi wa Taifa kwa kuhamasisha maendeleo. Tangu wakati huo, mwenge umekuwa ukikimbizwa katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo kupitia mbio hizo hamasa kubwa imetolewa ili kuendelea kudumisha amani, na kujenga uzalendo, umoja na mshikamano. Katika kipindi chote hicho, mbio za mwenge zimekuwa na mafanikio makubwa yanayosadifu maono ya waasisi wa Taifa letu.
Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2025 zinabeba kauli mbiu isemayo “Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu” ambayo inalenga kuwakumbusha na kuwasisitiza Watanzania wote kutumia kikamilifu haki yao ya kikatiba ya kushiriki Uchaguzi Mkuu kwa amani na utulivu.
Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2025 unatarajiwa kukimbizwa kwa muda wa siku 195, katika Mikoa 31 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo Serikali itafikisha ujumbe kwa wananchi na kuhamasisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo kwa kutembelea, kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi ya maendeleo.
Uzinduzi wa Mbio za Mwenge kwa Mwaka 2025 umehudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Dotto Biteko, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mussa Azzan Zungu, Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhandisi Zena Said, Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu, Viongozi wa Mahakama, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Vyama vya Siasa pamoja na Wananchi kutoka maeneo mbalimbali.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwasili katika Uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha mkoani Pwani kwaajili ya kuzindua Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa Mwaka 2025 leo tarehe 02 Aprili 2025.

default
Kikundi cha Watoto wa Halaiki wakifanya maonesho mbalimbali wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa Mwaka 2025 iliyofanyika Uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha mkoani Pwani leo tarehe 02 Aprili 2025.
Wakimbiza Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2025 wakiingia katika Uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha mkoani Pwani tayari kwa kuanza zoezi la kukimbiza Mwenge wakati wa Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 uliyofanyika Kibaha mkoani Pwani tarehe 02 Aprili 2025.

default
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa Mwaka 2025 katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha mkoani Pwani leo tarehe 02 Aprili 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwasha Mwenge wa Uhuru kuashiria uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa Mwaka 2025 katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha mkoani Pwani leo tarehe 02 Aprili 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akimkabidhi Mwenge wa Uhuru kiongozi wa Mbio za Mwenge kwa Mwaka 2025 Bw. Ismail Ali Ussi mara baada ya kuzindua Mbio hizo katika Uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha mkoani Pwani tarehe 02 April 2025
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiagana na Viongozi na Wananchi mbalimbali mara baada ya Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa Mwaka 2025 katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha mkoani Pwani leo tarehe 02 Aprili 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2025 Bw. Ismail Ali Ussi wakati wa Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa Mwaka 2025 katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha mkoani Pwani leo tarehe 02 Aprili 2025.