Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) Mhe. Halima Mdee imeielekeza Ofisi ya mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum katika mradi wa ujenzi wa shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa mkoa wa Morogoro.
Mhe. Mdee ameyasema hayo mara baada ya ziara ya kukagua miradi miwili ambayo
ni ujenzi wa nyumba za Wakuu wa Idara na mradi wa ujenzi wa shule ya Sekondari Wasichana ya Mkoa wa Morogoro katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro vijijini.
“wote tumetembelea ujenzi wa shule tumeshuhudia Kazi nyingi sana hazijakamilika Kwa kiwango ambacho fedha zimetolewa, Kamati ya Bunge inafanya kazi na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kama jicho letu uje ufanye ukaguzi Maalum katika mradi huu” amesisitiza.
Amesema hali ya miundombinu iliyojengwa katika mradi huo hauendani na thamani ya fedha ambayo Serikali imekwishatoa katika mradi huo.
Aidha, Kamati imemuelekeza Afisa Masuuli kuwasilisha Kwa Mkaguzi Mkuu wa Serikali Taarifa ya kina inayohusu matumizi ya fedha zote za mradi huo.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. Atupele Mwambene amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI imechukua maelekezo yote yaliyotolewa na Kamati hiyo na kwenda kuyasimamia katika utekelezaji.