
Na Gideon Gregory, Dodoma.
Leo Machi 27,2025 Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma imewafikisha mbele ya baraza hilo watumishi Sita wa umma kwa kosa la ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma ambapo wameshindwa kuwasilisha tamko la rasilimali na madeni kwa Kamishna wa Maadili.
Waliofikishwa mbele ya Baraza hilo ni madiwani wawili wa halmashauri ya Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, Mwandei Mohamed (Mtimbwani) na Mussa Buhero (Mayomboni) pamoja na Msajili wa Hati Msaidizi Mkoa wa Tanga, Mwajuma Kihiyo.
Vigogo hao wamefikishwa mbele ya Mwenyekiti wa Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Mstaafu Rose Teemba na kusomewa mashitaka yao ambapo wote wamekiri kutowasilisha tamko hilo.
Katika mashtaka hayo, upande wa Sektarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, umeongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Emma Geleni ambaye amesaidiana na Hassan Mayunga, Lidya Mwakibete na Hilary Hassan.
Katika baraza hilo, walalamikiwa kwa nyakati tofauti wamedaiwa kutowasilisha matamko ya raslimali na madeni kama kinavyoelekeza kifungu cha 9(1B) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na hivyo kukiuka kifungu cha 16(A) cha sheria hiyo.

Walalamikiwa wote kwa nyakati tofauti walitiwa hatiani kwa shtaka hilo baada ya kukiri kutowasilisha tamko hilo wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya uongozi kwa umma.
Akisoma mashtaka mbele ya Diwani Mwandei, Wakili Emma alileza kuwa mlalamikiwa huyo aliingia katika uongozi kwenye uchaguzi wa mwaka 2020, ambapo mwaka huo aliwasilisha tamko la raslimali na madeni lakini mwaka 2021 hakuwasilisha.
Alipoulizwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji Mstaafu Teemba, diwani huyo alikiri na baraza lilimtia hatiani kwa kukiuka Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma adhabu iliyomwendea pia Diwani Buhero baada ya kuonekana makosa yao yakishabihiana.
Kuhusu Hakimu Mziray, Wakili Mayunga amesema hakimu huyo amekuwa kiongozi tangu mwaka 2010 lakini ameshindwa kutimiza matakwa ya sheria ya kuwasisha tamko la raslimali na madeni kwa miaka mitatu mfululizo ambayo ni mwaka 2022 hadi 2023.
Alipoulizwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji Mstaafu Teemba alikiri kutowasilisha tamko hilo na hivyo baraza kumtia hatiani huku Msajili wa Hati Msaidizi wa Mkoa wa Tanga Mwajuma ametiwa hatiani kwa kutokuwasilisha tamko la raslimali na madeni kwa miaka miwili 2022 na 2023 wakati alishika nafasi hiyo 2020.
Tofauti na washitakiwa wengine Mwajuma ambaye muda wote alikuwa amejiinamia katika ukumbi huo wa baraza,hali iliyoonyesha hofu ya kujutia kosa lake na kutopenda kuonyesha uso wake kwa watu waliokuwa ndani ya ukumbi.
Kwenye malalamiko yanayomuhusu Columba Baraza limemtia hatiani baada ya kukiri kutowasilisha tamko lake kama anavyopaswa kwa mujibu wa sheria kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo ambayo ni 2022 na 2023.
Hata hivyo Columba amesema kuwa kumbukumbu zinamuonyesha kuwa alijaza fomu za tamko hilo kwa mwaka 2022 lakini hana hati ya kuthibitisha na kwa upande wa mwaka 2023 alichelewa kujaza fomu hizo lakini alipoulizwa zaidi ya mara tatu alikiri kutojaza ndipo Jaji Mstaafu Teemba alihitimisha kuwa, “Umekiri mwenyewe hukujaza fomu kwa wakati uliotakiwa, baraza litaendelea na utaratibu unaotakiwa, unaweza kwenda.”
Kwa upande wa mlalamikiwa Mhina, Wakili Lidya amedai kuwa Mhina katika mwaka 2022 na 2023 hakuwasilisha tamko lake la raslimali na mali kama Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inavyotaka.
Akijitetea Mhina amesema anakubaliana na maelezo hayo na kuwa kosa hilo limetokana na changamoto katika njia ya utumaji wa fomu hizo zilizojitokeza hapo awali lakini baada ya kuanza kutumika kwa utaratibu wa kujaza kwa njia ya mtandao kosa hilo halitajitokeza tena.
Baraza hilo limehairishwa mpaka kesho Machi 28,2025 saa 3 kamili asubuhi.



