AFISA Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA),Bw. Alban Kihulla,akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 25, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.
AFISA Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA),Bw. Alban Kihulla,akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 25, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
KATIKA kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita,Wakala wa Vipimo (WMA),imepanga kuhakiki Vipimo 3,923,652 vitumikavyo katika Sekta mbambalimbali nchini na imefanikiwa kuhakiki vipimo 3,668,149 sawa na asilimia 94 ya lengo.
Hayo yamesemwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA),Bw.Alban Kihulla,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan leo Machi 25, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.
“Kati ya vipimo hivyo vilivyohakikiwa, vipimo 102,969 vilikutwa na mapungufu ambayo yalirekebishwa na kuruhusiwa kuendelea kutumika na vipimo 5,607 vilikataliwa kutumika baada ya kuonekana na mapungufu ambayo hayarekebishiki.”amesema Bw.Kihulla
Aidha amesema kuwa katika kuunga mkono kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, Wakala imefanya ukaguzi na uhakiki wa vipimo kwenye mitungi ya gesi ili kuhakikisha kuwa wanunuzi wa gesi wanapata kiasi sahihi kulingana na thamani ya fedha wanayolipa kwa ajili ya huduma hiyo.
Amesema kuwa katika eneo hilo, Sheria ya Vipimo Sura 340 inawataka wauzaji wote wa mitungi ya gesi kuwa na mizani zilizohakikiwa na Wakala wa Vipimo, ili mnunuzi ajiridhishe na uzito wa gesi anayonunua.
“Nitoe rai kwa wauzaji wote wa gesi nchini, kuhakikisha wanatumia mizani zilizohakikiwa na WMA kwenye biashara ya gesi. Lakini pia niwaombe sana wanunuzi wa Nishati hiyo kuhakikisha kiasi cha gesi wanachopokea kwenye mitungi kupitia Mizani hiyo iliyohakikiwa na WMA”amesema
Hata hivyo amesema kuwa Wakala imeendelea kujenga na kukarabati majengo ya ofisi zake ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi, lakini pia kuwawezesha watumishi wanaotoa huduma hizo kuwa katika mazingira mazuri ambayo yataboresha utendaji wa watumishi hao.
Katika kipindi cha miaka minne Wakala imejenga majengo mapya ya ofisi katika Mkoa wa Mara na Simiyu. Vile vile ujenzi wa ofisi hizo umefanyika katika Mkoa wa Dodoma kwa kujenga Ofisi zinazotumika kama ofisi za Wakala wa Vipimo Makao Makuu.
Amesema kuwa utekelezaji wa ujenzi wa jengo ambalo sasa linatumika kama ofisi za Wakala wa Vipimo Makao Makuu ulianza Julai, 2022 na kukamilika March, 2025. Jengo hilo lina ghorofa nne, Vyumba 60 vya ofisi, kumbi 2 za mikutano na Maabara mbili.
” Jengo la WMA Makao Makuu lipo eneo la Medeli Mkoani Dodoma na limejengwa kwa gharama ya Billion 6.99 fedha zilizotokana serikali yetu inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”amesema
Hivyo amesema kuwa kukamilisha kwa ujenzi wa jengo hilo, Wakala wa Vipimo imejipanga kuendelea kuboresha mazingira ya ofisi kwa kujenga ofisi mpya katika Mikoa ya Lindi, Songwe, Ilala (Dsm) na Arusha kwa kutumia mapato ya ndani.
Pia amesema kuwa Wakala imefanikiwa kuhakiki idadi kubwa ya matenki ya magari yabebayo vimiminika shughuli ambayo inafanywa kupitia kituo kikubwa cha uhakiki wa vipimo cha Misugusugu.
Amesema kuwa Kituo hicho ni moja ya vituo vya kisasa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ambacho kinauwezo wa kupima matenki ya malori 60 kwa siku.
” Ongezeko la idadi ya matenki ya malori yaliyohakikiwa yamepelekea kurahisisha kiasi kikubwa cha mafuta kuondoka kwenye maghala na kiasi cha mafuta yanayosafirishwa kwenda nje ya nchi na mikoa mbalimbali kuondoka kwa haraka kwakuwa magari yanatumia muda mfupi katika uhakiki wake.”amesisitiza
Amesema kuwa muda mfupi unaotumika katika uhakiki wa matenki ya malori ya kusafirishia mafuta umepelekea kukua kwa biashara na kuondoa malalamiko kwa wadau ukilinganisha na muda mwingi uliokuwa unatumika awali.
“Katika kipindi cha Mwaka 2021 hadi Februari, 2025 Kituo cha Misugusugu kimefanikiwa kuhakiki tenki 21,746 ambapo, tenki hizi ndizo hutumika kusafirisha shehena ya vimiminika toka Bandari ya Dar es Salaam na kwenda mikoani au nchi za nje kama vile Zambia, Rwanda, Malawi, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.”amesema
Hata hivyo amesema kuwa pamoja na uwepo wa kituo kikubwa cha upimaji wa matenki ya malori katika eneo la Misugusugu Wakala ina vituo saidizi katika mkoa wa Mtwara, Iringa, Mwanza na Mkoa wa Kivipimo Ilala.
Aidha amesema kuwa WMA inaendela kutoa huduma za uhakiki wa kiasi cha mafuta (Jamii ya Petroli na Mafuta ya Kula) yanayoingia nchini kupitia bandari za Dar es salaam, Tanga na Mtwara.
“WMA imefanikiwa kuhakiki jumla ya lita 30,645,930,571 za mafuta kwa meli 546 zilizowasili nchini, kukiwa na ongezeko la meli 136 mwaka 2021/22 hadi meli 174 hadi kufika Februari,2025. Ongezeko hilo limetokana na maboresho yaliyofanywa na Serikali katika utoaji wa huduma na miundombinu ya bandari. “amesema
Pia amesema kuwa maboresho hayo yalijumuisha kusimika mita za kisasa katika Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara na kupelekea kuongezeka kwa ujazo wa mafuta yaliyohakikiwa kufikia jumla ya lita 30,645,930,571, ambapo lita 13,888,897,421 kwa ajili ya matumizi ya ndani (local) na lita 16,757,033,150 zilisafirishwa nje ya nchi.
Amesema kuwa taarifa na takwimu zinazopatikana kutokana na uhakiki wa vipimo na usimamizi wa matumizi sahihi ya vipimo katika biashara ya mafuta unaofanywa na WMA, zinatumiwa na taasisi mbalimbali za Serikali katika kufanya maamuzi. Taasisi zinazonufaika na taarifa hizo.