Featured Kitaifa

WAZIRI SIMBACHAWENE : WATENDAJI WAKUU WA SERIKALI ACHENI KUWAONA WAKAGUZI WA NDANI KAMA MAADUI

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene akikabidhiwa tuzo ya kuthamini mchango kwa Wakaguzi wa ndani kutoka kwa Rais wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani, Dkt. Zelia Njeza wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan baada ya kufungua Mkutano wa tatu wa Wakaguzi wa Ndani wa Sekta ya Umma

Na. Lusungu Helela – MWANZA

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene amewataka  Watendaji Wakuu pamoja na Bodi ya Wakurugenzi  kuacha kuwachukulia Wakaguzi wa Ndani  kama maadui badala yake wawape ushirikiano ili Taasisi zao zisipate  hati chafu.

Amesema kumekuwa na kasumba iliyojengeka kwa Watendaji wengi wa Serikali ya kuwaona Wakaguzi hao wa Ndani kama sio Watumishi na wapo pale kwa ajili ya kuharibu mipango yao ilhali wao ni watu muhimu na jicho la Taasisi.

Mhe.Simbachawene ametoa kauli hiyo leo jijini Mwanza wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kufungua Mkutano wa tatu wa Wakaguzi wa Ndani wa Sekta ya Umma.

Amesema Mtendaji  yeyote wa Serikali  anayewatumia vizuri Wakaguzi wa Ndani hawezi kuingia kwenye matatizo ya ubadhirifu wa fedha za umma huku akisisitiza kuwa Wakaguzi hao wapo kwa ajili ya kumsaidia yeye na Taasisi anayoiongoza.

“Acheni kuwaona Wakaguzi wa Ndani kama wageni na watu wasiotakiwa kwenye maeneo yenu ya kazi badala yake watumieni ili kuhakikisha fedha za umma zinatumika  kwa ajili ya miradi ya maendeleo iliyokusudiwa.

Amesema Wakaguzi wa ndani wanatekeleza jukumu nyeti la kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa busara, uwazi na kwa madhumuni sahihi. ” Bila kazi yenu, serikali haiwezi kufanya kazi kwa ufanisi” amesisitiza Simbachawene .

Katika hatua nyingine, Mhe.Simbachawene amewataka Wakaguzi hao kuhakikisha wanapata mafunzo ya mara kwa mara ili waweze kuendana na mabadiliko ya matumizi ya kidijitali katika ukaguzi wa fedha hususani katika matumizi ya akili mnemba (AI).

Ameongeza kuwa  ” Dunia inabadilika, teknolojia imeleta mageuzi ya jinsi tunavyofanya kazi, na kwa hiyo ukaguzi wa ndani na vyombo vya usimamizi wa taasisi navyo vinapaswa kubadilika.

Amesema matumizi ya mifumo hiyo imechangia mageuzi makubwa kwenye taasisi za serikali yenye hatua kubwa zaidi dhidi ya wanaobainika na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Ameongeza kuwa kesi vikubwa zimechunguzwa na viongozi waliothibitika kuhusika, wameachishwa kazi, wameshtakiwa na fedha zilizochotwa wamezirejesha, akisema huo  ni ujumbe wa wazi kwamba utumishi wa umma ni kuwatumikia watu na sio wa kujinufaisha.

Amesema Serikali  imedhamiria kuwa na mfumo wa kuhakikisha  rasilimali zinasimamiwa ipasavyo. 

Kwa upande wake, Rais wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani,  Dkt. Zelia Njeza amesema mahudhurio ya Wakaguzi wa Ndani  ni mazuri lakini kwenye ngazi ya Halmashauri yamekuwa hafifu hali inayochangia wataalamu hao kukosa mafunzo na hivyo kuendelea kufanya makosa yale yale kwenye kaguzi zao.

Amesema mkutano huo utafanyika kwa muda wa siku tano ambapo zaidi ya washiriki 800 watajifunza mbinu mbalimbali za ukaguzi ikiwemo  matumizi ya akili mnemba kwenye ukaguzi na hii inatokana na mabadiliko makubwa yanayotokea duniani kote katika ukaguzi wa fedha za umma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene akikabidhiwa tuzo ya kuthamini mchango kwa Wakaguzi wa ndani kutoka kwa Rais wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani, Dkt. Zelia Njeza wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan baada ya kufungua Mkutano wa tatu wa Wakaguzi wa Ndani wa Sekta ya Umma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene akizungumza wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan baada ya kufungua Mkutano wa tatu wa Wakaguzi wa Ndani wa Sekta ya Umma 

Rais wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani, Dkt.  Zelia Njeza akizungumza kabla ya kumakribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene kuzungumza na Wakaguzi wa Ndani  wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan baada ya kufungua Mkutano  huo wa tatu jijini Mwanza

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene (katikati) akiwa ameongoza na  baadhi ya wenyeji wa Mkutano wa tatu wa Wakaguzi wa Ndani kwa ajili ya kufungua mkutano huo wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan unaofanyika jijini Mwanza. Kulia ni Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Sengerema , Mhe. Senyi Ngaga na kushoto ni Rais wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani,  Dkt. Zelia Njeza

About the author

mzalendoeditor