Na Mwandishi Wetu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amemtaka Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Pwani, Mhandisi Leopold Runji, kuhakikisha wakandarasi wanakamilisha ujenzi wa barabara za lami Ikwiriri ndani ya miezi miwili ili wananchi wanufaike na maboresho ya miundombinu hiyo yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Mhe. Mchengerwa ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hizo wilayani Rufiji.
“Natoa miezi miwili tu, barabara ziwe zimekamilika ifikapo Mei 30, 2025, ikiwa ni pamoja na mitaro na taa za barabarani. Hakutakuwa na nyongeza ya muda,” amesisitiza Waziri Mchengerwa.
Ameagiza Meneja wa TARURA kuwasimamia wakandarasi wafanye kazi usiku na mchana, akibainisha kuwa barabara hizo zilipaswa kukamilika Desemba 2024 na iwapo hazitakamilika kwa muda uliopangwa, atamuwajibisha meneja huyo.
Nao, Baadhi ya wananchi, akiwamo Dereva wa bodaboda Ramadhan Mwipi na Mama Lishe Mariam Hamza, wamemshukuru Waziri Mchengerwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha barabara hiyo, wakieleza kuwa imeleta ahueni kubwa kwa usafiri na biashara zao.