Featured Kitaifa

SHULE YA MSINGI MKOKA YAIOMBA SERIKALI,WADAU KUSAIDIA VYUMBA VYA MADARASA

Written by mzalendoeditor

 
‎Dodoma, Kongwa

‎Shule ya Msingi Mkoka, kitengo maalum cha wanafunzi wenye mahitaji maalum, imetoa wito kwa serikali na wadau mbalimbali kuongeza msaada wa vyumba vya madarasa kutokana na changamoto ya upungufu wa vyumba hivyo. Shule hiyo kwa sasa ina wanafunzi 122, wakiwemo wasichana 65 na wavulana 57, lakini inatumia vyumba vya madarasa manne pekee. Hii inawalazimu wanafunzi wa madarasa matatu kushirikiana darasa moja, hali inayovuruga mazingira ya kujifunza.

‎Akizungumza wakati wa ziara ya Umoja wa Wanawake Viongozi katika Utumishi wa Umma Tanzania (ESWLT), Mkuu wa Shule hiyo, Furaha Mwashilandi, alieleza changamoto wanazokutana nazo, akisema hali hiyo inawapa walimu ugumu mkubwa wa kufundisha.

‎ “Ukosefu wa vyumba vya madarasa unaathiri sana utendaji wetu kama walimu na pia ustawi wa wanafunzi. Tunahitaji msaada wa haraka kuimarisha mazingira ya kufundishia,” alisema Mwashilandi.

‎Mbali na tatizo la madarasa, shule hiyo pia inakabiliwa na uhaba wa vifaa vya kufundishia na walimu wenye utaalamu wa kuwahudumia watoto wenye mahitaji maalum. Hasa, alisisitiza hitaji la vifaa maalum vya wanafunzi viziwi, ambao hutegemea mbinu za kuona katika kujifunza.

‎Ziara ya Umoja wa Wanawake Viongozi Tanzania ililenga kusaidia juhudi za serikali kwa kutoa msaada wa vifaa vya kufundishia, vyakula, vyandarua, taulo za kike, na sabuni kwa wanafunzi wa shule hiyo. Mwenyekiti wa Umoja huo, Justina Mashiba, aliahidi hatua zaidi za kuboresha mazingira shuleni hapo, ikiwemo ukarabati wa vyoo, uanzishaji wa matumizi ya gesi kupikia, na kuwapatia wanafunzi bima ya afya.

‎”Tunajitahidi kuunga mkono juhudi za serikali. Watoto hawa wanahitaji mazingira bora zaidi ya kufundishia na kujifunzia ili waweze kufikia ndoto zao,” alisema Mashiba.

‎Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mayeka Saimon Mayeka, aliwapongeza wadau kwa juhudi hizo huku akiwahamasisha wazazi wa watoto wenye mahitaji maalum kuhakikisha wanawapa mahitaji yao ya msingi badala ya kuwatenga.

‎”Hawa ni watoto wetu, na ni jukumu letu kama jamii kuhakikisha wanapata fursa sawa za elimu,” alisema Mayeka.

‎Shule ya Msingi Mkoka imeendelea kuwa kimbilio muhimu kwa watoto wenye changamoto mbalimbali za kiafya, ikiwemo viziwi, walemavu wa viungo, watoto wenye usonji, na wenye ulemavu wa akili. Hata hivyo, changamoto zilizopo, kama uhaba wa miundombinu na vifaa maalum, zinaendelea kudhoofisha maendeleo ya watoto hawa.

‎Shule ya Msingi Mkoka imeendelea kuwa kimbilio kwa watoto wenye mahitaji maalum ikiwemo viziwi,walemavu wa viungo, wenye usonji na watoto wenye ulemavu wa akili huku changamoto zilizopo zikiendelea kuathiri ustawi wa wanafunzi.









About the author

mzalendoeditor