Na Mwandishi Wetu Chemba, Dodoma
Wananchi wa kata ya Goima wilayani Chemba mkoani Dodoma wameelezea furaha yao kufuatia ujenzi wa daraja la mawe katika korongo la Igunga ambalo limekuwa ni kikwazo cha mawasiliano kwa muda mrefu katika kata hiyo.
Daraja hilo linalojengwa katika barabara ya Goima-Igunga-Hamai ni sehemu ya utekelezaji wa progamu ya uondoaji vikwazo katika barabara kupitia mradi wa RISE chini ya TARURA kwa mkopo nafuu toka Benki ya Dunia.
Mwenyekiti wa kijiji cha Igunga, Bw. Juma Salim Bakari amesema kuwa korongo hilo lilikuwa likiwakwamisha kwenye masuala ya usafiri na usafirishaji katika kata mbili za Goima na Hamai.
“Ujenzi huu ukikamilika nafikiri tutafaidika kwa mambo mengi ikiwemo suala la usafiri kutoka Igunga kwenda Hamai, ambako itarahisha hususani wagonjwa wanaopewa rufaa kutoka zahanati yetu ya Igunga kwenda katika Kituo cha Afya huko Hamai upande wa pili wa hili daraja”.
“Vilevile, vijiji vilivyopo ng’ambo huku upande wa Chemba, Milambo, Goima, Igunga na Jejeruse vitafaidika kufanya mawasiliano kupitia daraja hili na vijiji vya Hamai, Jinjo, Churuku, Itoro na Murungia”, amefafanua.
Aidha, Bw. Bakari amebainisha kuwa litakapokamilika daraja hilo litawezesha magari makubwa ya mizigo na abiria na kuwarahisishia wakulima wanaolima ng’ambo ya pili kusafirisha mazao yao kwa urahisi na gharama nafuu.
Kwa upande wake, mkazi wa kijiji cha Igunga, Bi. Ashura Juma Kusai ameelezea matarajio yake baada ya kukamilika kwa daraja hilo kuwa ni suluhu kwa akina mama waliokuwa wanapata shida kuzifikia huduma za afya ya uzazi katika Kituo cha Afya Hoima.
Naye, Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Chemba, Mhandisi Stewi Emmanuel amesema kuwa lengo la mradi huo ni kuondoa kikwazo katika barabara hiyo ambacho kilikuwa kinasumbua wananchi kwa muda mrefu na kuongeza kuwa Serikali kupitia TARURA iliamua kujenga daraja hilo la mawe lenye urefu wa mita 25 kumalizia tatizo hilo.