Serikali imeendelea kufanya juhudi za kuimarisha na kuweka mikakati bora ya kukuza Tasnia ya Maziwa kwa kutambulisha Mradi mpya wa Kimageuzi wa Tasnia hiyo.
Akizungumza katika Warsha hiyo ya kutambulisha Mradi wa Kimageuzi wa Tasnia ya Maziwa iliyofanyika leo Machi 17, 2025 mkoani Dodoma katika Ukumbi wa Hoteli ya Rafiki, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe, amesema Mradi huu utagharimu kiasi cha Dola 174.36 za Kimarekani na ni muhimu sana kwa watanzania wengi.
“tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kuwepo kwa Mradi huu” amesema Prof. Shemdoe
Aidha, Prof. Shemdoe ameelekeza kuwa Mradi huo uzingatie thamani ya fedha, muda pamoja na matokeo chanya yanayolenga kuwanufaisha vijana, wakina mama pamoja na makundi maalum
Vilevile, Prof. Shemdoe ameeleza kuwa Mradi huo ni Muunganiko wa Tanzania Bara na Visiwani unaotarajiwa kufika katika Mikoa 10 na Wilaya 28.
Prof. Shemdoe amewashukuru wadau wa maendeleo pamoja na wadhamini ambao ni IFAD, OPEC Fund, AFD, Irish League of Credit Union’s Foundation (ILCUF), HEIFER, International Tanzania (HI), Tanzania Agricultural Development Bank (TADB) na FAO.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo – Zanzibar, Ndg. Ali Khamis Juma, amesema Mradi huo unategemewa kuinua kipato na maisha ya Mtanzania hususani kwa wafugaji kwani Seerikali imejipanga kushirikiana na wafugaji wadogo na kuwasaidia kukua katika tasnia ya Maziwa.
Pia, Mkurugenzi wa Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ndg. Stephen Michael, amesema Maziwa yanachangia kwa asilimia 30% ya pato la Taifa, japo kunahitajika kuhakikisha upatikanaji wa Maziwa unatakiwa kuwekewa Mazingira mazuri ikiwemo kuboresha Malisho na upatikanaji wa maji, Huduma za Ugani, Tafiti, mafunzo na Masoko kwa ajili ya wafugaji.
Naye, Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Prof. George Msalya amesema Tasnia ya Maziwa ina changamoto nyingi zikiwemo Uzalishaji mdogo wa Maziwa, Masoko na ukusanyaji wa Maziwa ambao unachangiwa sana na mabadiriko ya hali ya hewa, kwa hiyo Mradi huu utaenda fanya Mageuzi makubwa kitasnia.